Mkuu wa Polisi Misri auawa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mlipuko wa bomu karibu chuo kikuu cha Cairo, Misri

Mkuu wa Polisi nchini Misri ameuawa na watu wengine watano kujeruhiwa wakati mabomu matatu yalipolipuka karibu na chuo kikuu cha Cairo.

Kundi linalojiita Ajnad Misr, au Askari wa Misri, limesema linahusika na shambulio hilo.

Mabomu mawili ya kwanza yalilipuka yakipishana kwa dakika moja, huku la tatu likifyatuka saa moja baadaye.

Kumekuwa na ongezeko la mashambulio ya kijeshi yakilenga taasisi za serikali tangu kundi la Muslim Brotherhood ling'olewe mwaka 2013.

Serikali ya Misri imesema wanamgambo wamekwishaua watu wapatao 500 tangu mwezi Julai mwaka jana, wengi wakiwa ni polisi na wanajeshi.

Wasiwasi umeongezeka kutokana na kuongezeka kwa ghasia wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa rais mwezi Mei, mwaka huu.

Kikundi cha Ajnad Misr kimetoa taarifa fupi kikisema kimefanya shambulio hilo kikiwalenga maafisa wa polisi ambao walihusika katika kuwaua waandamanaji wengi.

Kikundi hicho ambacho hakifahamiki sana kimesema shambulio hilo pia limekuja ikiwa ni kulipiza kisasi kutokana na kuwekwa kizuizini waandamanaji wengi wanawake.

Milipuko ya Jumatano imetokea karibu na kituo cha polisi wa kutuliza ghasia nje ya lango kuu la kitivo cha uhandisi katika chuo kikuu cha Cairo.

Tangu kung'olewa madarakani kwa Rais Mohammed Morsi anayehusishwa na kikundi cha Muslim Brotherhood-zaidi ya watu 1,000 wameuawa na maelfu ya wafuasi wa kikundi hicho wamekamatwa katika msako ulioendeshwa na mamlaka za serikali.