Mwandishi wa AP auawa Afghanistan

Image caption Kathy Gannon(kushoto) na Anja Niedringhaus(kulia) kwa msomaji ameuawa Afghanistan.

Mwandishi mmoja wa habari mwanamke wa shirika la habari la Associated Press ameuawa kwa kupigwa na afisa wa polisi mashariki mwa Afghanistan, huku mwingine akijeruhiwa.

Mmoja wa wanawake hao, Anja Niedringhaus mwenye umri wa miaka 48 raia wa Ujerumani, ameuawa katika shambulio hilo. Mfanyakazi mwenzake, Kathy Gannon raia wa Canada mwenye umri wa miaka 60, ameripotiwa kuwa hali yake inaendelea vizuri baada ya kujeruhiwa.

Anja ambaye alikuwa mwandishi mpiga picha amefanya kazi katika maeneo mbalimbali yenye migogoro ya kivita ikiwa ni pamoja na Yugoslavia, Afghanistan, Ukanda wa Gaza, Israel, Kuwait na Uturuki.

Kathy ni mwandishi maalum wa shirika la Associated Press katika nchi za Pakistan na Afghanistan.

Shambulio hilo limefanyika katika mji wa Khost karibu na mpaka wa Afghanistan na Pakistan.

Tukio hilo limekuja wakati Afghanistan ikiimarisha ulinzi kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais Jumamosi ikiwa ni kukabiliana na vurugu za wapiganaji wa Taliban.