Wataka waandishi wa aljazeera kuachiwa

Image caption Ni maandamano ya wafanyakazi wa Al-Jazeera mjini London wakipinga kushikiliwa kwa waandishi wao nchini Misri

Mashirika ya vyombo vya habari yamerejelea wito wa kutaka kuachiliwa huru kwa waandishi watatu wa habari wa shirika la al-Jazeera ambao wamekuwa wakishikiliwa kwa siku 100 sasa tangu wakamatwe nchini Misri.

Waandishi hao watatu, akiwemo mwandishi wa habari wa zamani wa BBC, Peter Greste, walifunguliwa mashitaka mwezi Februari, wakituhumiwa kusambaza habari za uongo na kukisaidia kikundi cha ugaidi.

Wamekana mashitaka hayo, ambayo al-Jazeera imeyaita kuwa ni "upuuzi."

Kesi hiyo imechochea shutuma kutoka vyombo vya habari vya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu duniani kote.

Waandishi hao watatu ni miongoni mwa watu 20 wanaokabiliwa na mashitaka kama yao. Ni watu wanane tu ambao mpaka sasa wako gerezani, ambapo wengine 12 wamesomewa mashitaka bila kuwepo mahakamani.

Mwandishi wa nne wa al-Jazeera, Abdullah al-Shami, ambaye anafanyia chaneli ya Kiarabu, anashikiliwa tangu mwezi Agosti bila ya kufunguliwa mashitaka.

Bwana al-Shami amekuwa katika mgomo wa kula na mke wake amesema afya yake inazorota.