Ballo mwimbaji taarab afariki dunia

Image caption Marehemu Muhammad Khamis Bhallo

Mwimbaji maarufu wa taarabu nchini Kenya Muhammad Khamis Bhallo amefariki dunia katika mji wa Mombasa nchini Kenya .

Marehemu Bhallo ambae amefia nyumbani kwake akiwa na umri wa zaidi miaka sitini, kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo hali ambayo ilimlazimu kwenda nchini India mara kadhaa kwa ajili ya matibabu.

Bhallo kwa zaidi ya miongo mitano alikuwa akitunga mashairi na vile vile kuimba nyimbo za mahadhi ya taarab na kujizolea sifa na wafuasi sio tu mjini Mombasa nchini Kenya, bali pia hata nje ya mipaka ya Kenya zikiwemo nchi nyengine za Afrika Mashariki na kati na hata nchi za Ulaya.

Mashabiki wake wengi walivutiwa zaidi na umahiri wake wa kutumia lafudhi ya Kiswahili cha Kimvita na kiamu.

Waliokuwa wakifuatilia kazi za Bhallo, watakumbuka jinsi mziki wake ulivyonoga katika miaka ya themanini na tisini pindi alipokuwa akilumbana na mpinzani wake Maulidi Juma na Bi Shakillah kutoka Tanzania.

Akitoka katika jamii yenye mapenzi makubwa ya filamu na nyimbo za kihindi, Bhallo aliweza kuzikonga nyoyo za wengi kwa kutafsiri baadhi ya nyimbo za kihindi na kuziimba kwa lugha ya Kiswahili.

Hata hivyo, kuzorota kwa hali yake ya afya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na tatizo la moyo, kulimtoa kabisa katika ulingo wa muziki na kusababisha kuzagaa kwa uvumi kwamba Bhallo alikwisha kufa siku nyingi, taarifa ambazo hazikuwa za ukweli kwani Bhallo amefariki dunia Jumapili na kuzikwa siku hiyo hiyo huko mjini Mombasa.