Wakimbizi wasomali wanaswa Nairobi

Image caption Mamia ya Wasomali wakamatwa katika msako Eastleigh

Uwanja wa michezo wa Kasarani unafahamika kwa michezo aina tofauti, iwe ni riadha ama kandanda.

Hata hivyo tangu wikiendi iliyokwisha , Uwanja wa Kasarani ndio umekuwa hifadhi ya mamia ya watu wanoshukiwa kuwa ni wakimbizi walionaswa katika msako mkubwa zaidi kuwahi kufanyika katika mji wa Nairobi katika miaka ya hivi punde.

Mamia ya polisi wamevamia eneo la Eastleigh viungani mwa mji mkuu wa Nairobi mahali wanakoishi maelfu ya wakaazi kutoka jamii ya Wasomali.

Image caption Mamia ya Wasomali wakamatwa katika msako Eastleigh

Hatua hiyo ya polisi wa Kenya imewadia baada ya kutokea milipuko ya mara kwa mara ya mobumu ya kujitengenezea pamoja na grenadi ambayo imesababisha maafa makubwa.

Polisi wanasema walichukua hatua hiyo baada ya kuwakamata raiya wa Somali ambao hawana stakabadhi rasmi za kuwaruhusu kuwa Kenya katika matukio ya hivi punde ya milipuko iliyosababisha vifo vya watu sita katika mtaa huo.

Mwandishi wa BBC Robert Kiptoo aliyepo Kasarani anasema kuwa msako huo wa Eastleigh umewanasa waliyomo na wasiokuwemo.

Miongoni mwa waliokamatwa ni wakimbizi wenye stakabadhi rasmi za shirika la umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR vile vile wasomali wenye asili ya Kenya lakini waliopatikana bila ya vitambulisho pia wamekamatwa.

Msemaji wa polisi Masoud Mwinyi amesema kuwa polisi wamepata vifaa na kemikali za kutengeza vilipuzi karibu na Madrassa moja mtaani Eastleigh.