UN yalaani mauaji ya maafisa wake

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wawili hao waliuawa katika eneo la Galkayo katika mpaka na Puntland

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay, ameshutumu mauaji ya washauri wawili wa Umoja wa Mataifa ambao wamekuwa wakifanyakazi katika kitengo cha Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

Washauri hao wawili wa kimataifa walikuwa Galkayo kusaidia jitihada za Ofisi ya UNODC katika eneo hilo wakati walipouawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika uwanja wa ndege wa Galkayo, Puntland, Somalia.

Umoja wa Mataifa umesema unawalaani wauaji hao.

"Wafanyakazi wenzetu wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakifanyakazi ya kuwasaidia wananchi wa Somalia kufikia ndoto yao ya kuwa na taifa lenye amani na imara. Hakuna uhalali wowote wa kufanyika shambulio hilo.

Natoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahalifu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria bila kuchelewa".Amesema Bwana Kay.

Haki miliki ya picha other
Image caption Nicholas Kay, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.

"Natoa salamu zangu za pole kwa familia na marafiki wa watu hao waliouawa.

Umoja wa Mataifa umedhamiria kuendelea na msaada wao wa dhati kwa wananchi wa Somalia ambao wanatoka katika mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa," amesema Mwakilishi huyo Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Kay.

Habari kutoka Mohadishu, Somalia, zinasema kikundi cha wapiganaji wa al-Shabab kimepongeza mauaji hayo na kudai kufurahishwa na taarifa hizo za kuuawa kwa raia wa kigeni katika mji wa Galkayo, katikati mwa Somalia Jumatatu.

"TUnapongeza na kufurahishwa na mauaji ya maafisa wa Umoja wa Mataifa, leo. Mashirika ya Umoja wa Mataifa daima ni maadui wa Waislam na Wasomali na vifo vyao vimelifurahisha kundi la wapiganaji wa Mujahdeen" wamesema.

Walipoulizwa kama wanahusika na mauaji hayo, al-Shabab wamesema kwa sasa hawapingi wala kudai kuhusika na mauaji hayo”