Ukraine yatoa saa 48 kwa wanaharakati

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji wa Ukraine wanaoiunga mkono Urusi wakiwa mbele ya jengo la serikali katika mji wa Donetsk

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine amewaonya wanaharakati wanaoipendelea Urusi ambao wameyateka majengo ya serikali katika miji ya mashariki kuanza mazungumzo ili kupata suluhisho la kisiasa au wakabiliwe na nguvu za kijeshi.

Bwana Arsen Avakov amesema hali hiyo itaweza "kupata ufumbuzi katika muda wa saa 48".

Mapema, baadhi ya wale waliokuwa wamejichimbia katika ofisi za maafisa usalama katika mji wa Luhansk tangu Jumapili wameondoka katika jengo hilo.

Umoja wa Ulaya, Urusi, Marekani na Ukraine wanatarajiwa kukutana wiki ijayo katika mazungumzo ya kwanza yatakayozihusisha pande hizo nne tangu kuzuka kwa mgogoro wa Ukraine.

Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza ukimya uliopo tangu Urusi ijinyakulie jimbo la Crimea la kusini mwa Ukraine mwezi Februari. Majeshi ya Urusi kwa sasa yamesambazwa katika mpaka wa mbili hizo za Ukraine na Urusi.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka tangu majengo ya serikali katika miji ya mashariki ya Ukraine ya Luhansk, Donetsk na Kharkiv kuchukuliwa na wanaharakati wanaopendelea Urusi JUmapili.

Bwana Avakov amesema operesheni dhidi ya magaidi ilikuwa inaendelea katika majimbo yote matatu na itakamilishwa katika muda wa siku mbili zijazo.

"kuna njia mbili," amewaambia waandishi wa habari, " suluhisho la kisiasa kupitia mazungumzo au matumizi ya nguvu ya kijeshi.