Wanamgambo wapuuza amri ya Ukraine

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanamgambo wa Urusi walioficha sura zao wakiwa wamesimama mbele ya bendera ya Urusi nje ya makao makuu ya jengo la wakala wa shirika la ulinzi la Ukraine

Wanamgambo wenye mwelekeo wa Urusi wanaodhibiti majengo ya serikali ya Ukraine mashariki mwa nchi hiyo, wameendelea kuyakalia majengo hayo, hivyo kupuuza amri ya kuwataka kuondoka kabla ya muda waliopangiwa kumalizika, la sivyo wataondolewa kwa nguvu na majeshi ya Ukraine.

Rais wa muda wa Ukraine alitoa kauli ya kutumika hatua za kijeshi iwapo majengo ya serikali hayataachiwa ifikapo saa mbili asubuhi.

Lakini waandishi wa habari wamesema bendera ya Urusi imeendelea kupepea katika kituo cha polisi cha Ukraine kilichotekwa katika jimbo la Sloviansk.

Mapigano kati ya watu wenye silaha wanaopendelea utawala wa Urusi katika vitongoji vya mji wa Sloviansk, Jumapili yalisababisha afisa mmoja wa Ukraine kuuawa.

Katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika Jumapili, Urusi imeitaka Ukraine kutotumia nguvu za kijeshi dhidi ya waandamanaji mashariki mwa Ukraine.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaliy Churkin, ameitaka serikali ya Ukraine "kuanza mazungumzo ya dhati".

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanaharakati wenye mwelekeo wa Urusi wakiwa na silaha katika mji wa Slavyansk

Urusi imeitaka Ukraine kusitisha "vita dhidi ya watu wake"

Lakini balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa Yuriy Sergeyev amesema Urusi imeanzisha mgogoro bandia mashariki mwa Ukraine.

Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema Jumatatu kuwa ina ushahidi kwamba majeshi ya Urusi yalikuwa nyuma ya "operesheni ya miji ya mashariki ya Ukraine kujitenga" na kwamba Ukraine itawasilisha ushahidi katika mkutano utakaofanyika Geneva baadaye wiki hii.

Ukraine iliahidi kutumia nguvu za kijeshi iwapo Warusi hawataondoka katika majengo ya serikali wanayoyakalia katika mji wa Sloviansk na miji mingine kadha.

Watu mashariki mwa Ukraine kwa sasa wanasubiri kuona endapo rais wa muda Olexander Turchynov atatumia jeshi kuyarejesha majengo yanayoshikiliwa na wanamgambo wa Urusi.