Oscar Pistorius amaliza kujitetea

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Oscar Pistorius anakana kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp

Upande wa mashitaka katika kesi ya mauaji dhidi ya Oscar Pistorius umemaliza kumhoji mwanariadha huyo.

Oscar aliyekatwa miguu yote miwili anakana kutekeleza mauaji hayo akisisitiza kwamba alidhani marehemu Steenkamp alikuwa jambazi aliyevamia nyumba mwake.

Anakabiliwa na kifungo cha kati ya miaka 25 au maisha gerezani, iwapo atapatikana na makosa ya mauaji ya kupangwa.

Kabla ya kuanza kusikizwa kesi hiyo, mwendesha mashitaka Gerrie Nel alisema kuwa alitumai kumaliza kumhoji mwanariadha huyo siku ya Jumanne.

Alimuomba Jaji Masipa aahirishe kesi wakati wa mapumziko ya pasaka hadi tarehe 5 Mei.

Ameeeleza kwamba mawakili wenzake wanakabiliwa na kesi nyengine 'nzito zaidi' wanazostahili kuzishughulikia pamoja na 'masuala ya kibinafsi'.

Haki miliki ya picha .
Image caption Pistorius akitoka mahakamani

Ombi hilo liliungwa mkono na upande wa utetezi, uliosema kwamba kesi hiyo inapaswa kumalizika tarehe 16 Mei kama ilivyopangwa. Jaji alisema atatoa hukumu yake ya ombi hilo siku ya Jumatano.

Siku ya Jumatatu, Bwana Nel alipendekeza kwamba Pistorius anajifanya kuzidiwa na hisia kuficha matatizo anayopata kujibu masuali mazito anayoulizwa.

Jaji Thokozile Masipa alisitisha kwa muda kesi hiyo mara mbili siku ya Jumatatu baada ya Pistorius kuanza kulia.

Muda mfupi kabla kesi kumalizika kwa siku, Nel alisema: " unazidiwa na hisia sasa kwa sababu unaudhika, kutokana na kuwa ushahidi wako huenda si wa kweli."

Mwendesha mashtaka huyo anayejulikana kwa mtindo wake wa kutishia watu anapowahoji, baadaye alimuuliza Pistorius: " Hautumii hisia zako kukwepa kujibu maswali?"

Pistorius alisema akili yake haikumanika kama inavyostahili wakati wa ufyetuaji risasi huo.

Haki miliki ya picha
Image caption Upande wa mashitaka umesema, kuwa Pistorius anatumia machozi yake kama sababy ya kutaka kuhurumiwa

Awali, kwa mara nyengine Nel alimdadisi kwa uzito Pistorius kuhusu wakati alipompiga Bi Steenkamp risasi.

Mwanariadha huyo alisisitiza kwamba hakuna na nia ya kumuua mtu yoyote, alisema: "Nilifyetua risasi kutokana na uoga."

Nel baadaye alisema kwamba Pistorius alibadili ushahidi wake kutoka kusema alikuwa akijikinga na hadi kusema kwamba alifyetua risasi kwa makosa.

Mwendesha mashtaka akasema hii ni kutokana na kuwa ukweli ni : "Ulimfyetulia Reeva risasi."

"Sio kweli," Pistorius akajibu, huku akibubujikwa kwa machozi na kuilazimu mahakama kusitisha vikao kwa muda.

Pistorius alisema yeye na marehemu Steenkamp walibarizi jioni pamoja kabla ashutuke usingizini kutokana na kusikia sauti iliyotoka bafuni.

Mashahidi wa upande wa mashitaka walieleza kusikia mwanamke aliyepiga mayowe, lakini upande wa utetezi unakana ushahidi huo.