Jeshi lawasaka wasichana walitotekwa Nigeria

Haki miliki ya picha Nigeria Army
Image caption Wanajeshi wanakabiliwa na wakati mgumu kuangamiza kundi la Boko Haram

Vikosi vya usalama nchini Nigeria vinawasaka wasichana mia moja waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kiislamu wa kundi la Boko Haram katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Borno.

Wasichana hao walikuwa wakifanya mitihani yao walipotekwa nyara .

Utekaji nyara huo umefanyika katika eneo ambalo kundi la Boko Haram kuendesha sana shughuli zake na kuna wasiwasi kuwa huenda wasichana hao wamepelekwa katika eneo la msituni katika jimbo hilo karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon.

Lori lililotumika kuwasafirishia wanafunzi hao, lilipatikana likuwa limeegeshwa kando ya barabara.

Duru zinasema kuwa wapiganaji hao wanafahamu vyema eneo hilo ambalo wamekuwa wakiendeshea harakati zao, na kwamba wanajeshi hawajaweza kuwafurusha kutoka katika maficho yao msituni

Seneta wa jimbo hilo Ali Ndume, ameiambia BBC kuwa lori kubwa lililotumiwa kuwabeba wasichana hao limepatikana na huenda sasa wasichana hao wanatembea kupitia msitu mmoja.

Msichana mmoja ameiambia BBC kwamba yeye na wenzake walifanikiwa kutoroka waliporuka kutoka kwenye lori hilo.