Mafuriko Dar: Watu 25 wathibitika kufa

Image caption Mafuriko Dar es Salaam, Tanzania

Watu 25 wamethibitika kufa mkoani Dar es Salaam nchini Tanzania kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo kuanzia Ijumaa hadi Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadik Meck Sadik amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo akisema watu wengine 14 wanadaiwa kufa, lakini hawajathibitishwa na polisi.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam wenye wilaya tatu, amesema watu 11 wamekufa katika wilaya ya Ilala, huku wengine wawili hawajaonekana mpaka sasa.

Taarifa kutoka wilaya ya Temeke imesema watu saba wamethibitishwa kufa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha.

Pia kuna taarifa za watu 21 kufariki dunia katika wilaya ya Kinondoni, japo hawajathibitishwa.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam Bwana Sadik amesema miundombinu ya barabara na madaraja imeanza kurejeshwa baada ya kuharibiwa na mafuriko na kusababisha mkoa wa Dar es Salaam kukosa mawasiliano ya ndani na pia kukosa mawasiliano na mikoa jirani.