Opresheni dhidi ya ugaidi yaanza Ukraine

Haki miliki ya picha AP
Image caption Opresheni dhidi ya ''ugaidi'' yaanza Ukraine

Kaimu rais wa Ukraine Olexander Turchynov amesema kuwa vikosi vya kijeshi vya Ukraine vimeuteka na kuuthibiti uwanja mmoja wa kijeshi katika eneo la Kramatosk mashariki mwa Ukraine, baada ya mapigano na makundi yanayounga mkono Urusi.

Rais huyo ameliambia bunge la taifa huko Kiev kuwa operesheni hiyo maalum inafanywa hatua kwa hatua.

Bwana Turchynov aliliambia bunge kuwa operesheni ya kukomboa miji na mali ya umma kutoka mikononi mwa ''Mgaidi'' itaendelea kuambatana na sheria za kibiniadamu.

Mamia ya watu wanaodaiwa kuwa wanaharakati wanaounga mkono Urusi wamekongamana nje ya uwanja huo wakiwafokea majeshi waliotua humo kutoka Kiev.

Makundi ya waasi wanaounga mkono Urusi wameteka takriban miji 10 katika mashariki mwa taifa hilo.

Image caption Opresheni dhidi ya ''ugaidi'' yaanza Ukraine

Duru kutoka Marekani zinasema kuwa maelfu ya majeshi ya Moscow yamezingira maeneo ya mpaka wa Ukraine na kuibua hofu ya uvamizi wakati wowowte iwapo Ukraine itaingilia kati katika miji hiyo iliyotekwa.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa Ukraine huenda ikatumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe iwapo kiev itaendelea na operesheni hiyo dhidi ya wananchi wake waasi.

Taarifa kutoka Kremlin zinasema kuwa Putin alitoa tahadhari hiyo katika mazungumzo ya simu na Kiongozi wa Ujerumani bi Angela Merkel.

Viongozi hao wanasemekana kuafikiana kuhusiana na umuhimu wa mkutano wa kwanza wa pamoja baina ya Bara Ulaya Urusi Ukraine na Marekani.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika huko Geneva Uswisi.

Miji iliyoko Mashariki mwa ukraine zinataka kura ya maoni kufanyika huko kuamua iwapo wanataka kuendelea kuwa sehemu ya Ukraine ama wangependa kuiga mfano wa Crimea iliyoamua kujitenga na kujiunga na Urusi baada ya utawala mpya kumng'oa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Victor Yanukovich.