Wasiwasi kuhusu wanafunzi waliotekwa Nigeria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boko Haram imekuwa ikifanya mashambulizi ya kuvizia huku jeshi likidai kuwa linakabiliana nao

Hali ya suitofahamu inakumba hali ya wasichana zaidi ya miamoja waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram Mashariki mwa Nigeria.

Jeshi linasema kuwa zaidi ya wasichana 100 wameweza kutoroka lakini wazazi wanasema kuwa wasichana wengi bado hawajulikani waliko.

Wapiganaji hao waliwateka nyara wasichana kutoka shule ya wabweni walipokuwa wanajiandaa kwa mitihani yao.

Duru zinasema ni wasichana 17 pekee waliofanikiwa kutoroka kinyume na kauli ya jeshi.

Inaanimika kuwa wapiganaji wa Boko Haram ndio wamewateka nyara wasichana hao na kuwapeleka katika msitu ulio karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon.

Kundi hilo linapiga vita serikali ya Nigeria likisema kuwa linataka nchi hiyo itawaliwe kwa misingi ya kiisilamu.

Jumatano watu 18 waliuawa katika shambulizi lililofanywa wilayani Gwoza Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Kilio cha wazazi

Haki miliki ya picha Nigeria Army
Image caption Wadadisi wanasema shambulizi dhidi ya wasichana ni jambo la aibu kubwa kwa serikali

Taarifa ya jeshi ilisema kuwa wasichana wengi walifanikiwa kutoroka ingawa wazazi wanakana madai hayo wakisisitiza kuwa wasichana wengi bado hawajapatikana

Kitendo cha shule ya mabweni kushambuliwa ni jambo la aibu kubwa kwa serikali la Nigeria wanaosema kuwa operesheni ya kijeshi dhidi ya wanamgambo hao inafanikiwa.

Masaa kadhaa kabla ya jeshi kutoa taarifa yake, gavana wa jimbo la Borno alisema kuwa idadi kubwa ya wasichana bado hawajapatikana na kutangaza zawadi ya dola laki tatu kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu wasichana hao.

Wanajeshi, polisi na vikosi vingine vya ulinzi pamoja na watu wa kujitolea wanahusika na msako wa wasichana hao.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ameelezea kushutushwa na shambulizi hilo na kutaka wasichana hao kuachiliwa mara moja.

"kuwalenga wasichana na watoto ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa,'' alisema Ban

"shule ni mahala panapopaswa kuwa salama kwa watoto kusoma na kukua. ''

Kundi hilo limekuwa likiwateka wasichana na wanawake kwa lengo la kuwatumia kama watumwa wa ngono.