Nigeria:Wazazi wawasaka watoto msituni

Image caption Shule ya mabweni iliyovamiwa huku wasichana zaidi ya miamoja wakitekwa nyara

Wazazi wa takriban watoto miamoja waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram wameingia msituni kuwatafuta watoto wao.

Wasichana hao walitekwa nyara kutoka shuleni mwao katika eneo moja la vijijini Kaskazini Mashariki mwa Nigeria Jumatatu usiku.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria anasema kuwa ni hatari sana kwa wazazi hao hata kutafakari kuingia msituni , kwani wapiganaji wa Boko Haram wamewaua mamia ya watu mwaka huu , kwa kuwakata vichwa vyao.

Rais Goodluck Jonathan, anakutana na magavana wa majimbo na maafisa wakuu wa jeshi kujadili swala la usalama.

Awali jeshi lilisema ni wasichana 18 pekee kati ya 129 waliotekwa nyara bado hawajapatikana .

Wengine wote walifanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa Boko Haram.

Lakini wazazi wanapinga kauli ya jeshi na wanasema kuwa wasichana wengi bado hawajulikani waliko.

Wapiganaji hao waliwateka nyara wasichana kutoka shule ya wabweni walipokuwa wanajiandaa kwa mitihani yao.

Duru zinasema ni wasichana 17 pekee waliofanikiwa kutoroka kinyume na kauli ya jeshi.

Inaanimika kuwa wapiganaji wa Boko Haram ndio wamewateka nyara wasichana hao na kuwapeleka katika msitu ulio karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon.

Kundi hilo linapiga vita serikali ya Nigeria likisema kuwa linataka nchi hiyo itawaliwe kwa misingi ya kiisilamu.

Jumatano watu 18 waliuawa katika shambulizi lililofanywa wilayani Gwoza Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Wadadisi wanasema shambulizi dhidi ya wasichana ni jambo la aibu kubwa kwa serikali

Taarifa ya jeshi ilisema kuwa wasichana wengi walifanikiwa kutoroka ingawa wazazi wanakana madai hayo wakisisitiza kuwa wasichana wengi bado hawajapatikana