Wasomali walaani marufuku ya Miraa UK

Image caption Wasomali walaani marufuku ya Miraa UK

Jamii ya wasomali waishio nchini Uingereza wanaotafuna mmea wa Miraa wameelezea hasira yao baada ya serikali ya Uingereza kuthibitisha kuwa itapiga marufuku kileo hicho .

Uingereza ni mnunuzi mkuu wa mmea wa Miraa Katika mataifa ya Magharibi.

Mmea huo unaokuzwa zaidi katika eneo la Afrika mashariki , hutafunwa zaidi na wasomali waishio nchini Uingereza .

Mwandishi wa BBC wa Idhaa ya Kisomali Rage Hassan alitembelea duka linalouza miraa saa 24 kaskazini mwa mji wa London kushuhudia hali ya watafunaji wa Miraa .

Wafanyi biashara wanasema kuwa kuiharamisha Miraa itawanyima kitega uchumi chao .

Zao la miraa linategemewa sana kiuchumi na wakulima wengi katika maeneo ya Meru na Embu nchini Kenya.

Iwapo itapigwa marufuku Uingereza itakuwa taifa la pili kuharamisha mmea huo baada ya Uholanzi kupiga marufuku uingizaji na uuzaji wa Miraa.

Majina.

Miraa pia Inafahamika kama Khat na mairungi kwa walaji.

Ni jani lenye dawa ambalo likitafunwa linatoa juisi ambayo ina visisimuzi vya asili na ni maarufu kwa jamii ya wasomali.

Kuna wasiwasi kuwa dawa zinaweza kusababisha maradhi ya akili au kuchanganyikiwa.

Serikali ya Uholanzi ilisema kelele, uchafu na tishio kwa umma linalotolewa na watu wanaotafuna mirungi kama baadhi ya sababu za kupiga marufuku dawa hiyo.

Image caption Wasomali walaani marufuku ya Miraa UK

Watumiaji wanajisikia wako macho, wana furaha na wanaongea sana.

Inakata hamu ya chakula.

Matumizi makubwa yanaweza kusababisha kukosa usingizi, shinikizo la damu, matatizo ya moyo na kukosa nguvu.

Inaweza kusababisha kansa ya mdomo ikiwa itatumika kwa muda mrefu.

Inaweza kusababisha kujiskia kuwa na wasiwasi, ukorofi na kusababisha hofu na matatizo ya akili.

Inaweza kusababisha matatizo ya akili kuwa makubwa zaidi.

Mumea huo kwa kiasi kikubwa unatafunwa na watu kutoka Somalia, Ethiopia, Kenya na Yemen.

Matumzi ya visisimuzi umepigwa marufuku Marekani, Canada na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya.

Lakini bado inapatikana Uingereza ambako inauzwa kihalali katika idadi ndogo ya maduka.

Mwaka uliopita ujumbe wa serikali ya Uingereza ilitembelea Kenya kubaini na kuchunguza ukuaji na uuzaji mbali na athari za Miraa.

Wabunge wa kenya pia walitembelea uingereza kuishawishi serikali ya nchi hiyo isipige marufuku Miraa kwani ni kitega uchumi cha mamilioni ya wakulima wanaotokea mkoa wa kati wa nchi hiyo ya Kenya.

Aidha kulikuwa na madai kuwa pato kubwa la mmea huo huenda linafaidi makundi ya kigaidi, hata hivyo hakukuwa na ushahidi wa kutosha kudhihirisha madai hayo.