Wanaharakati wa Urusi watoa masharti

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanaharakati wa Urusi nchini Ukraine

Wanaharakati wanaiounga mkono Urusi wametangaza masharti mapya ambayo wanahitaj yatekelezwa kabla ya wao kuondoka kutoka kwa majengo ya serikali ya Ukraine ambayo wamekuwa wakiyadhibiti.

Mwakilishi wa wanaharatakati wanaounga mkono Urusi kwenye mji wa mashariki mwa Ukrain Donetsk, Alexander Gnezdilov, ameiambia BBC kuwa hawataondoka kwenye majengo ya serikali hadi pale serikali aliyoitaja kuwa ya mapinduzi itakapoondoka madarakani

Mawaziri wa mashauri ya nchi za kigeni kutoka Urusi, Ukraine, Muungano wa Ulaya na Marekani wamekubaliana kwamba makundi haramu ya wanamgambo yaliyo nchini Ukraine ni sharti yavunjwe, kisha yaweke silaha chini na kuondoka katika majengo ya serikali.

Akiongea kwenye kikao cha dharura cha bunge waziri mkuu wa Ukrain Arseny Yatsenyuk amesema kuwa makubaliano yaliyoafikiwa mjni Geneva yana maanisha kuwa wale waliotwaa majengo ni lazima waondoke mara moja.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry ametaja mazungumzo hayo ya siku ya Alhamisi kuwa kazi ya siku njema lakini akizungumza mjini Washington saa kadhaa baadaye, Rais Obama ametilia shaka kujitolea kwa Urusi kutekeleza makubaliano hayo.

Bwana Obama amesema yeye pamoja na viongozi wa ulaya watabuni mikakati ya kuiwekea urusi vikwazo zaidi endapo Moscow haitatekeleza makubaliano hayo.