Rais wa Korea Kusini alaumu nahodha

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Juhudi za uokozi zingali zinaendelea

Rais wa Korea kusini Park Geun Hye amemkosoa nahodha na wafanyikazi wa Feri ya abiria iliozama kwa kuikimbia feri hiyo na hivyobasi kufananisha vitendo vyao na mauaji.

Matamshi ya rais Park yanafuatia uchapishaji wa mawasiliano kati ya feri hiyo na waokozi ,yaliobaini kwamba kulikuwa na hali ya wasiwasi mbali na kutokuwepo mpangilio wa uokozi.

Idadi ya watu waliofariki imeongezeka na kufikia 64 huku watu 238 wakiwa hawajulikani waliko,wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule.

Wapiga mbizi wanaendelea na juhudi za kutafuta mili ya watu waliozama na feri hiyo huku wakijitahidi kuingia ndani ya feri yenyewe.

Habari zilizotangazwa kuhusu mawasiliano ya mwisho kati ya wafanyakazi wa Feri iliyozama Korea Kusini na maafisa wa kudumisha usalama baharini zinaonyesha kuwa kulitokea hali ya wasiwasi kabla ya mkasa huo, ambayo huenda ilichangia pakubwa vifo vya abiria wengi katika feri hiyo.

Taarifa hiyo mpya ilitolewa Jumapili alasiri wakati ambapo imethibitishwa kuwa maiti 62 zimepatikana kwenye mabaki ya feri hiyo, na kufanya idadi ya watu waliothibitishwa kufariki kufikia 58. Zaidi ya watu 240 hawajulikani waliko hivi sasa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jamaa wa waathiriwa walikabiliana na polisi wakilaumu waokozi kwa kujikokota

Jamii za watu ambao hawakuwa wamepatikana walifanya maombi ya Pasaka Jumapili katika chumba cha kufanyia mazoezi katika eneo la Jindo, ambako mamia ya watu wamekusanyika tangu feri hiyo kupinduka wakisubiri habari kuwahusu wapendwa wao.

Mama mmoja alisema kuwa watoto waliofariki walikuwa wakitunzwa vizuri.

"Naamini watoto hao wako mbinguni ," mama huyo alisema.

Jung Maria, mwanamke aliyejitolea kuzisaidia familia za walioathirika, alisema kuwa jamaa za watu wasiojulikana waliko wanapaswa kusikia kilichotokea kwa njia moja au nyingine.

"ikiwa wamefariki, tunapaswa kupata miili yao haraka iwezekanavyo. Na iwapo kutatokea muujiza basi turejeshewe watoto hao upesi pia, alisema mfanyakazi huyo wa kujitolea

Idadi kubwa ya abiria katika meli hiyo walikuwa wanafunzi wa shule ya upili waliokuwa wakienda kwenye mojawapo wa kisiwa kubarizi. Hadi kufikia sasa kumekuwa kungali kuna ubishi mkubwa iwapo nahodha mwenyewe alikuwa ameshikilia sukani.