Sudan Kusini:Mauaji ya kikabila Bentiu

Image caption Waasi nchini Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa unasema kuwa vikosi vinavyoipinga serikali nchini Sudan Kusini viliwaua mamia ya watu kwa sababu ya kabila lao wakati vilipouteka mji wa Bentiu wiki jana.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo, watu hao walilengwa wakiwa katika maeneo salama walikokuwa wanahifadhiwa kama vile msikitini, makanisani na hospitalini.

Umoja huo umesema kuwa watangazji katika baadhi ya vituo vya redio walitumia lugha ya chuki na uchochezi na kuwataka watu wa kabila fulani kuondoka mjini humo huku wakiwashauri wanaume kuwabaka wanawake.

Watu wa kabila laNuer, ni wafuasi wakubwa wa kiongozi wa waasi na makamu wa zamani wa Rais Riek Machar

Wapiganaji wanaomuunga mkono makamu wa rais wa zamani Riek Machar waliuteka mji wa Bentiu ambao ni mji mkuu wa jimbo la Unity siku sita zilizopita.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walilaani kile walichokitaja kama mauaji yanayowalenga raia kwa misingi ya ukabila.

Rais Salva Kiir anatoka kabila la Dinka ambalo ndilo kabila kubwa kuliko yote nchini Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umesema kuwa watu ambao hawakuwa wa kabila la Nuer,waliuawa Bentiu.