Urusi yadai Ukraine inakiuka mkataba

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa Ukraine wanaounga mkono Urusi

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ametuhumu maafisa wakuu wa Kiev kwa kuvunja mkataba uliofikiwa wiki jana mjini Geneva kusuluhisha mgogoro wa Ukraine.

Alisema kuwa serikali ya Muda ya Ukraine , ambayo haitambuliwi na Moscow, haijachukua hatua zozote kuwapokonya silaha makundi haramu hasa wapiganaji wazalendo.

"wapiganaji wenye itikadi kali ndio wenye kauli kuu,'' alidai waziri huyo akilaani kitendo cha mashambulizi yaliyotokea Mashariki mwa Ukraine.

Pia alilaani maandamano yanayoendelea katika barabara ya Maidan mjini Kiev.

Mapema Jumapili, watu watatu waliuawa baada ya kushambuliwa kwa bunduki katika kizuizi cha barabarani kinachodhibitiwa na wapiganaji wa Ukraine wanaounga mkono Urusi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ukraine imedaiwa kutositisha ghasia

Hali iliyosababisha tukio hilo bado haijajulikana. Watu wanaotaka kujitenga na Ukraine walisema kuwa shambulizi hilo lilifanywa na wapiganaji wazalendo wa Ukraine.

Mkataba unavyokiukwa

Hata hivyo serikali ya Ukraine ilitaja shambulizi hilo kama uchokozi unaofanywa na wanajeshi wa Urusi.

Tarehe 17 mwezi Aprili, mkataba wa Geneva, ulifikiwa katika mazungumzo yaliyoshirikisha Urusi, Ukraine na Muungano wa Ulaya na Marekani.

Mkataba huo ulitoa wito wa kusitishwa kwa ghasia Mashariki ya Ukraine na kutoa wito kwa makundi haramu kusalimisha silaha zao na kuondoka kutoka majengo ya serikali.

Wapiganaji wanaounga mkono Urusi, bado wanadhibiti majengo ya serikali katika miji tisa katika jimbo la Donetsk mashariki mwa Ukraine.

Bwana Lavrov alisema ombi kubwa la makubaliano ya Geneva lilikuwa kuzuia ghasia zozote, lakini ombi hilo halizingatiwi na Ukraine.