Mcheza densi asababisha vurugu Brazil

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hawa ni baadhi ya waandamanaji katika mojawapo ya maandamano ya kupinga Serikali 2013.

Kumezuka mapigano kati ya jeshi la polisi na wakaazi wenye hasira usiku kucha katika mojawapo ya viunga vya mji mkuu Rio de Janeiro.

Barabara zimefungwa mjini humo wakati risasi zikisikika kutoka eneo hilo na polisi waking'ang'ana kuwadhibiti wakaazi hao.

Ghasia hizo zilianza kufuatia kifo cha mwanamume mwenye umri wa miaka 26, Douglas Rafael da Silva, mchezaji densi wa kulipwa.

Kulingana na familia yake mwili wake ulipatikana ukiwa umejaa vidonda na waliwalaumu maafisa wa polisi kwa kumpiga hadi kufa baada ya kumshuku kuwa mwanachama wa genge moja linalouza madawa ya kulevya.

Watu walikusanyika katika lango la kuingia katika makaazi hayo ya mabanda alikopatikana mtu huyo akiwa ameauwa na wakataka kujua kutoka kwa maafisa wa polisi sababu za kuuliwa kwake.

Polisi kadhaa wa kijeshi wenye silaha wako mahali hapo kufuatia habari kuwa kituo cha polisi kilichoko mahali hapo kimevamiwa.

Pavaozinho ni mojawapo ya makaazi ya mabanda ambayo Serikali Kuu ya Brazil imejaribu kuwatimua magenge ya walangunzi wa madawa ya kulevya wenye silaha kutoka kwa jamii na kueneza amani na mmalaka ya polisi.

Polisi wamekiri katika mahojiano na BBC kuwa wameshindwa kuthibiti usalama katika makaazi ya mabanda katika mji mkuu wa Rio de Jenairo, muda mfupi tu wakati ambapo wageni wengi wanatarajiwa nchini humo, kukiwemo maelfu wanaotarajiwa nchini kwa sababu ya Kombe la Dunia.