Bomu laua afisa wa polisi Misri

Image caption Polisi wa Misri mjini Cairo

Afisa mwandamizi wa polisi wa Misri ameuawa katika mlipuko wa bomu mjini Cairo.Brigedia Jenerali Ahmed Zaki aliuawa wakati kilipuzi klipowekwa chini ya gari lake rasmi kilipofyatuliwa katika kitongoji cha 6 October City cha magharibi mwa mji mkuu wa Cairo.

Ni polisi wa tano wa ngazi ya jenerali kuuawa tangu mwaka huu kuanza.

Wapiganaji wa Jihad wameongeza mashambulio dhidi ya maafisa usalama na kuwaua mamia tangu jeshi limwondoe madarakani Rais Mohammed Morsi mwezi Julai mwaka jana.

Vyanzo vya habari za kiusalama nchini Misri vimeiambia Idhaa ya Kiarabu ya BBC kwamba afisa mwingine pia aliuawa Jumatano wakati akiwafuatilia "magaidi" katika mji wa Alexandria.

Jumamosi, watu wenye silaha alimuua afisa usalama na polisi mmoja wakati akifanya doria katika barabara inayounganisha mji wa Cairo na mji wa mfereji wa Suez.

Shambulio hilo limefanyika siku moja baada ya polisi mmoja kuuawa katika shambulio lingine la bomu mjini Cairo lililodaiwa kufanywa na kikundi cha Ajnad Misr (askari wa Misri).

Kikundi hicho kimesema na kampeni ya kulipiza kisasi dhidi ya polisi kwa sababu ya msako wa serikali dhidi ya wafuasi wa chama cha Bwana Morsi cha Muslim Brotherhood, ambapo zaidi ya watu 1,300 wameuawa na wengine 16,000 kukamatwa.

Mashambulio hayo yanatishia usalama wakati huu wa maandalizi ya uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi Mei, ambapo mkuu wa majeshi ya Misri wa zamani Abdul Fattah al-Sisi anatarajiwa kushinda.

Mwanajeshi huyo mstaafu, field marshal al-Sisi ameapa kuvitokomeza vikundi vya wapiganaji nchini Misri.