Zambia yaomboleza kifo cha Liwewe

Jamii ya Wanamichezo hususan Soka nchini Zambia inaomboleza Kifo cha Mtangazaji Gwiji wa soka nchini humo Mzee Dennis Liwewe ambaye aliwahi kuwa Mwandishi wa habari wa Michezo wa BBC, idhaa ya Kiingereza katika Kipindi cha Focus on Africa.Erick David Nampesya ameandaa makala kuhusiana na kifo cha Mtangazaji huyo Nguli.

Serikali ya Zambia imetangaza siku tatu za Maombolezo kwa heshima ya Nguri huyo wa Utangazaji ambaye alikuwa na utangazaji wenye hamasa kwa soka la Zambia ambao ulisababisha asafiri zaidi ya mara 96 katika nchi arobaini na mbili duniani akiwa na Timu ya taifa ya soka ya Zambia.

Liwewe alishirikishwa na Kundi la Sakala Brothers nchini humo katika wimbo wa kuipongeza Timu ya Taifa ya soka ya Zambia mwaka juzi baada ya kutwaa Ubingwa wa Afrika nchini Gabon akiwahimiza kutobweteke na kuzidi kukaza msuli kwa maendeleo ya soka la Zambia.

Mzee Dennis Liwewe ambaye alifariki hapo juzi akiwa na umri wa miaka 78, alifanya kazi ya Utangazaji soka kwa Zaidi ya miaka 50,kabla ya kustaafu mwaka 1993 kwa ushauri wa madaktari kutokana na mshtuko wa moyo alioupata kufuatia ajali ya ndege iliyouwa wachezaji wote wa timu ya taifa ya Zambia mwezi April 28,mwaka 1993,ambapo yeye alinusurika ajali hiyo baada ya kuchelewa ndege hiyo iliyokuwa ikielekea nchini Senegal.

Utangazaji wake wenye hamasa na uzalendo mkubwa ulimfanya atambulike na kuheshimiwa nchini Zambia ambapo alichukuliwa mmoja wa watu wenye umaarufu mkubwa,ambapo alikuwa na urafiki mkubwa na Viongozi wakuu nchini humo wakiwemo Marais wa zamani wa nchi hiyo.

Katika Wimbo huu Puteni Chimwela Mzee Dennis Liwewe anahimiza wadau wa soka nchini humo kuunganisha nguvu kwa pamoja na kufanya juhudi ili kuleta maendeleo ya mchezo huo unaopendwa na wengi duniani kote.

Dennis Liwewe alihusisha maisha yake ya kila siku na mchezo wa soka ambapo katika moja ya utani alivyojenga uhusiano na mkewe ambaye sasa ni mjane Bi Sylvia aliwahi kuufananisha na hali 18 za mechi kali ya soka ambapo alisukuma mashambulizi makali akitumia mtindo wa 5-3-2 ili kumshawishi Bi Sylvia,ambapo hata hivyo ngoma ilikuja kugonga besela siku moja baada ya mkewe kususia mtoko aliokuwa ameandaa yeye na marafiki zake,Lakini akaongeza kuwa alijipanga upya na ngoma kuanza kuzunguka uwanjani na hatimaye Sylvia akawa ndani ya himaya yake kwa maisha ya ndoa iliyoendelea kudumu hadi wiki hii Kipo kilipowatenganisha kutokana na matatizo ya Ini

Na hivi karibuni akiwa mgonjwa alimweleza mwandishi wa habari wa BBC aliyemtembelea nyumbani kwake mjini Lusaka,akisema kuwa angenyayuka kitandani kwa mtindo wa 4-4-2,na kuongeza kuwa kama ingelazimu dakika za nyongeza kabla ya mikwaju ya Penalt basi alikuwa tayari katika kuendelea kupigania uhai wake,lakini kwa mapenzi ya Mungu Kipenga kilipulizwa hapo juzi jumanne kabla ya dakika za nyongeza.

Kwa Heri Mzee Dennis Liwewe.