G7 kuiwekea Urusi vikwazo zaidi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption wanamgambo wanaeondelea kuyadhibiti majengo ya serikali mashariki mwa Ukraine.

Viongozi wa nchi zenye uwezo mkubwa duniani G7 wamekubaliana kuiwekea vikwazo zaidi Urusi, wanayosema inaendelea kuchochea ghasia mashariki mwa Ukraine.

katika taarifa yao, viongozi hao walionyesha wasiwasi wao kuhusu jitihada za wanaharakati wanaounga mkono Urusi kuendelea kuyumbisha mashariki mwa Ukraine.

Urusi ,wamesema haijachukua hatua zozote kutekeleza makubaliano ya mjini Geneva mbali na kuwaamrisha wanamgambo hao kuondoka katika majengo ya serikali wanayodhibiti.

Hatahivyo viongozi hao wameipongeza Ukraine kwa kujizuia katika kukabiliana na makundi ya wanamgambo yaliojihami.

Wakati huohuo, wanamgambo wanaounga mkono Urusi mashariki mwa mji wa Ukraine wa Slavianski wamelitekanyara kundi moja la wachunguzi 13 wa kimataifa pamoja na wale wa Ukraine ambao walikuwa wanazuru eneo hilo wakiwa miongoni mwa ujumbe unaoshirikishwa na shirika la usalama la muungano wa Ulaya.

Kundi hilo linashirikisha wachunguzi wa kijeshi wa Ujerumani pamoja na wawakilishi wa Denmark,Poland,Sweden na jamhuri ya Czech.

Kiongozi mmoja anayeunga mkono Urusi amesema kuwa wachunguzi hao wamezuiliwa kwa kuwa mpelelezi mmoja wa serikali ya Ukraine alikuwa miongoni mwao.

Ujerumani imesema kuwa itatumia njia zote za kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa wamewachiliwa huru.

Na huku hali ya wasiwasi ikipanda,Marekani imesema kuwa imegundua kwamba ndege za kijeshi za Urusi zimekuwa zikiingia katika anga ya Ukraine katika kipindi cha masaa 24 yaliopita.