Marekani yaiomba Urusi kuhusu waangalizi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption John Kerry wa Marekani na mwenzake Sergei Lavrov wa Urusi.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry ameiagiza Urusi kutumia ushawishi wake ili kuona kuwa waangalizi wa kijeshi waliotekwanyara mashariki mwa Ukraine wanawachiliwa huru.

Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Urusi ,bwana Kerry ameonyesha wasiwasi wake kuhusu kile alichokitaja kama hatua ya uchokozi ya majeshi ya Urusi kuelekea karibu na mpaka wa Ukraine.

Wanadiplomasia wengine wa magharibi pia wametoa wito kwa Urusi kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa maafisa hao 13 wanaozuiliwa katika mji wa Sloviansk wameachiliwa.

Wale wanaowazuia waangalizi hao wamesema kuwa huenda wakatolewa baada ya majeshi ya Ukraine kuwaachilia huru wafungwa inaowazuia.

Wanamgambo wanaoendelea kudhibiti majengo ya serikali katika mji huo wanasema kuwa miongoni mwa wachunguzi hao ni wapelelezi wa Ukraine.

Kwa Upande wake waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov amesema kuwa Ukraine ni sharti isitishe oparesheni zake za kijeshi katika eneo la mashariki mwa Ukraine kama hatua za haraka za kumaliza hali ya wasiwasi iliopo.