Utata kuhusu Heroine iliyonaswa Kenya

Image caption Hiki ni kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kunaswa Afrika

Serikali ya Kenya imelalamika kuwa haikupewa taarifa zozote kuhusu dawa za kulevya zilizonaswa na wanajeshi wa Australia wanaoshika doria katika ufuo wa bahari Hindi , ufukweni mwa Kenya.

Hii ilijitoza katika mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina Mohammed na balozi wa Australia nchini humo Bwana Geof Tooth aliyetakiwa na serikali kuelezea kuhusu tukio la kunaswa kwa dawa hizo.

Dawa hizo zenye uzani wa kilo 1,023 ambazo ni kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kunaswa katika pwani ya Afrika, ni za thamani ya dola milioni 289.

Zilinaswa Ijumaa zikiwa zimepakiwa katika mifuko 46 ambayo ilikuwa imefichwa kwenye mifuko ya Simiti

Ubalozi wa Australia umekanusha madai kuwa, manowari yake ya kijeshi iliingia katika eneo la bahari inayomilikiwa na Kenya na kunasa shehena ya dawa hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, ubalozi huo umesema kuwa madawa hayo ya kulevya yalinaswa katika eneo la bahari inayomilikiwa na jamii ya kimataifa na kuwa hakuna manowari yake iliyoingia Kenya.

Pia yalinaswa katika operesheni dhidi ya biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya. Taarifa zilisema kuwa dawa hizo ziliharibiwa kwa kumwagwa baharini.

Taarifa hiyo imesema kuwa tukio hilo halina uhusiano wowote na Kenya na kuwa habari zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini Australia kuwa madawa hayo yalinaswa karibu na kenya ilikuwa kutoa taswira tu ya eneo la tukio.

Shehena kubwa kuwahi kunaswa

Wiki iliyopita wanajeshi wa Australia walinasa mashua moja iliyokuwa imesheheni zaidi ya tani moja ya madawa ya Heroine katika bahari ya hindi na taarifa hiyo inasema kuwa mashua iliyonaswa haikuwa na usajili wowote.

Ubalozi huo umekariri kuwa haukuhusika na operesheni hiyo ambayo ilifanywa na wanajeshi wa majini wa Australia wanaoshika doria katika bahari ya hindi chini ya mkataba wa kimataifa wa kupambana na uharamia na uhalifu katika bahari ya hindi.

Hata hivyo ubalozi huo umesema kuwa shirika la kimataifa la kupambana na uharamia na uhalifu CMF litaendelea kushirikiana na serikali ya Kenya hasa katika kuelezea zaidi operesheni yake.

Tangu shehena hiyo kukamatwa kumekuwa na shauku miongoni mwa maafisa wa ulinzi na wale wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo na madai kuwa kenya haikuhusishwa katika operesheni hiyo licha ya kutendeka katika eneo linalosemekana kuwa lake.