Makombora yatikisa Damascus, Syria

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maelfu wa wakimbizi wa Syria wanakumbwa na hali ngumu huku vita vikiendelea

Msururu wa makombora yamevurumizwa katikati mwa mji wa Damascus, na kuwauwa watu 12 huku hamsini wakijeruhiwa.

Shirika la habari la Syria limesema kituo kimoja cha ufundi na hata shule zimeshambuliwa .

Kadhalika shirika hilo limesema waasi ndio waliofanya shambulio hilo.

Serikali imekuwa ikishambulia maeneo yanayokaliwa na waasi karibu usiku na mchana.

Shambulizi hili linakuja siku moja baada ya rais Bashar Assad kusema atasimama kugombea tena uongozi wa nchi hiyo akiipuuza wito wa jamii ya kimataifa kuwa ajiondoe madarakani ili kutafuta suluhu la vita vya syria.

Wanajeshi wamewaondoa wapiganaji kutoka maeneo mengi waliyokuwa wanadhibiti na yanayozingira mji mkuu Damacus, lakini wakazi wanasema wapiganaji hao wamezidisha mashambulizi ya roketi na makombora mjini Damascus.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Assad anatarajiwa kushiriki uchaguzi mkuu unaokuja

Neno magaidi linatumiwa na maafisa wakuu wa Syria, kuwalenga wale wanaopigana kuiangusha serikali ya Rais Assad.

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria linasema kuwa idadi ya majeruhi katika vita hivyo huenda ikaongezeka.

Zaidi ya watu 150,000 wameuawa katika vita hivyo vilivyodumu miaka mitatu sasa.

Mamilioni ya wengine wamelazimika kutoroka makwao huku mapigano yakiendelea kutokota.

Wengine zaidi ya milioni tatu na nusu wanaosa msaada muhimu ikiwemo dawa na chakula.