Tigo yazindua Facebook ya Kiswahili

Haki miliki ya picha reuters
Image caption Tigo inasema huduma hiyo ya Facebook itaweza kutumika bila malipo

Kampuni ya Simu za mkononi ya Tigo nchini Tanzania imezindua matumizi ya mtandao wa kijamii wa mawasiliano ya Facebook,kwenye mfumo wa lugha ya Kiswahili huku kukiwa hakuna malipo.

Mfumo huo ambao ni wa kwanza kwa watumiaji nchini humo unaelezwa kuwa utawezesha watumiaji mbali mbali hasa wale wasiofahamu lugha ya Kiingereza kuwasiliana kwa njia hiyo ya Facebook.

Mtandao huu wa Facebook kupitia kampuni ya simu za mkononi ya Tigo unaelezwa kuwa umelengwa kuwafaidisha watumiaji wa simu za mkono kujiunga kwa kutumia lugha ya Kiswahili tofauti na ilivyo sasa ambapo ili kujiunga na Facebook lazima kutumia lugha ya Kiingereza.

Meneja wa uzalishaji bidhaa wa Kampuni ya Tigo William Mpinga n nasema kuwa wameamua kuzindua mfumo huo kama jitihada zao za kuwaingiza wateja katika ulimwengu wa Digital na pia kuzidi kuipanua lugha ya Kiswahili Duniani kote ambako unapatikana mtandao wa facebook.

Kwa Mujibu wa Bwana William Mpinga ni kwamba mtumiaji mtandao huo wa facebok,akiwa na line ya tigo akiishajiunga na mtandao wa facebook basi ataweza kuendelea kuwasiliana kwa njia hiyo ya mtandao hata kama atakuwa ameishiwa salio la kawaida kwa matumizi ya simu kwa sababu huduma hiyo ya mtandao inapatikana bure.

Kwa upande wa watumiaji mbali mbali wa mtandao niliozungumza nao wameeleza kuwa mbali na kufaidi mtandao huo kwa mawasiliano lakini pia wameeleza kuwa lugha ya Kiswahili itawaongezea urahisi zaidi wa kuwasiliana na pia kuweza kutangaza bidhaa mbali mbali na hivyo kuweza kujiongezea kipato huku wakitumia mtandao huo wa facebook kwa kibiashara Zaidi ya mawasiliano pekee.