Hasira kwa kukamatwa wanablogu Ethiopia

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wanablogu wa Zone 9

Hatua ya serikali ya Ethiopia kuwakamata wanablogu 9 imezua hasira kwenye mitandao ya kijamii

Wanablogu haomaarufu nchini Ethiopia walikamatwa mwishoni mwa wiki huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akitarajiwa kuzuru nchi hiyo.

Mnamo siku ya Ijumaa saa kumi na moja jioni , simu za wanablogu 9 zilianza kulia bila kukoma.

Pia walipata ujumbe mwingi tu wa barua pepe

Ujumbe ulikuwa kwamba mmoja wa kikundi cha wanablogu tisa, kijulikanacho kama Zone 9 alikuwa amekamatwa, huku wengine wakipata onyo kali.

Lakini inaonekana onyo lilikuja mapema mno. Wanablogu wengine watano na wandishi habari watatu pia walikua wamekamatwa.

Wote tisa bado wanazuiliwa huku polisi wakifanya uchunguzi kwamba wanablogu hao walikuwa wanashirikiana na mashirika ya kigeni , wanaharakati wa kutetea haki za binadamau na kutumia mitandao ya kijamii kuhatarisha usalama wa nchi.

Bila shaka kukamatwa kwa wanablogu hao, kunaonyesha hali ya kisiasa ilivyo nchini humo na jukumu la mitandao ya kijamii katika siasa za nchi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakilalamika kuhusu ukosefu wa uhuru wa kujieleza nchini Ethiopia.

Vituo vingi vya televisheni na radio vinamilikiwa na serikali.

Kwa sababu ya hali hii nchini Ethiopia , wanaharakati wengi pamoja na wanablogu wamekuwa wakitawala mitandao ya kijamii na blogu ili kuweza kutoa maoni yao kuhusu kinachoendelea nchini humo na pia kuelezea hasira yao kufuatia kukamatwa kwa wanablogu hao.

Wanablogu wa Zone 9, waliungana miaka miwili iliyopita na kuanza kutumia mitandao kukosoa serikali wakiituhumu kwa kukiuka haki za binadamu na kujenga miundo msingi duni.

Duru zinasema kuwa msako wa serikali ni jibu lake kwa taarifa ya kundi hilo iliyowekwa kwenye mtandao wa Facebook kuwa wataanza tena harakati zao kwenye blogu hiyo baada ya miezi kadhaa ya kusitisha shughuli zao.