Nigeria kufunga Shule na Ofisi Jumatano

Image caption Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathana ameagiza shule zote na ofisi za serikali katika mji mkuu wa Abuja nchini humo zifungwe wakati wa siku tatu za Mkutano wa Uchumi wa Dunia World Economic Forum utakaanza nchini humo jumatano ijayo.

Serikali imesema hatua hiyo ni kuarahisisha misafara ya magari. Lakini suala la kuimarisha ulinzi huenda ni mambo yaliyosababisha hatua hiyo Mwandishi wa BBC Will Ross anasema akiwa Abuja.

Ulinzi mkali umehaidiwa kwa wageni wapatao 1000 wakati wa mkutano huo.

Rais Jonathan amesema polisi wapatao 5000 na wanajeshi watafanya doria na kushika hatamu za ulinzi wakati wa mkutano huo utakaoanza wiki ijayo.

Waziri Mkuu wa China Li Keqiang na Marais wa Rwanda, Senegal na Kenya ni miongoni mwa viongozi wa juu wa nchi watakaohudhuria.

Mji wa Abuja katika siku arobaini zilizopita ulishambuliwa kwa matukio mawili ya mabomu yaliyoua watu wapatao tisini.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Baadhi ya wanawake wakiandama kutaka serikali kuchukua hatua zaidi kuwaokoa wasichana waliotekwa

Kundi la Boko Haram linadaiwa kuhusika na mashambulizi hayo.

Kundi hilo hilo pia linatuhumiwa kuwateka nyara wasichana zaidi ya 200 katika shule moja kwenye mji wa Borno uliopo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria siku arobaini zilizopita.

Jina la kundi hilo lenye tafsiri ya "Kupiga marufuku elimu ya nchi za Maghiribi" kwa lugha ya Kihausa kimekuwa kikiendesha mashambulizi kadhaa kaskazini mwa Nigeria katika siku za hivi karibuni.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanawake walivaa nguo nyekundu kuonyesha kuguswa na wasichana waliotekwa

Inakadiriwa watu wapatao 1500 wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na kundi hilo pamoja na operesheni ya majeshi ya serikali wakati wa kulisaka kundi hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry ambaye anafanya ziara barani Afrika amesema Marekani itafanya kila liwezekanalo kuisaidia serikali ya Nigeria kuwaokoa na kurudisha nyumbani wasichana mia mbili waliotekwa na kundi la waislamu linalosadikiwa kuwa la Boko Haram siku kumi tisa zilizopita.