Goodluck aahidi wasichana watapatikana

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amezungumza wazi kwa mara ya kwanza kuhusu kutekwa kwa waschana takriban 200 wa shule kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Katika taarifa yake ya kwanza hadharani tangu wasichana 200 kutekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Waislamu wenye itikadi kali wa Boko Haram, Rais Goodluck Jonathan, amesema kuwa kila juhudi zinapaswa kufanywa kuwakomboa wasichana hao.

Tangazo la Rais lilitolewa kufuatia shinikizo zilizotolewa na familia, makundi ya wanawake na watu wengine ambao wameitaka Serikali kufanya bidii zaidi kuhakikisha kuwa wasichana hao wanakombolewa.

Rais alisema kuwa maafisa wa usalama wamekuwa wakitafuta kila mahali wakitumia ndege na helikopta lakini akakiri kuwa hawajafaulu kutambua walikofichwa wasichana hao.

Haki miliki ya picha AFP

Alisema kuwa Serikali yake imelazimika kuomba msaada katika kuwatafuta wasichana hao kutoka Serikali za Marekani, Uingereza na Uchina.

Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana na kundi hilo la wapiganaji tangu mwaka 2009, lakini mashambulizi na milipuko ya mabomu yameendelea kusikika kila mahali bila kukoma.

Hivi majuzi kumekuwa na milipuko katika mji mkuu wa Abuja katika muda wa majuma matatu ambapo karibu watu 90 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Mnamo Jumatano Kongamo la Dunia juu ya Uchumi wa Afrika utafanyika mjini Abuja na swala la usalama limewatia maafisa wa usalama tumbo joto, ambapo imetangazwa kuwa siku hiyo shule zote na afisi za Serikali zitafungwa ili kuimarisha usalama eneo hilo la mkutano.