Kisanga cha mahabusu kuvua nguo TZ

Image caption Ramani ya Tanzania

Mahabusu wa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha, kaskazini mwa Tanzania, Jumanne walisababisha vurugu katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini humo baada ya kuvua nguo na kugoma kushuka kwenye basi lililowachukua kwenda mahakamani wakipinga kitendo cha watuhumiwa wawili wa dawa za kulevya kuachiwa huru.

Watuhumiwa wanaolalamikiwa ambao mashtaka yao yalibadilishwa mara mbili ili wapewe dhamana ni Dharam Patel na Nivan Patel wanaodaiwa kukamatwa na kete 173 za heroini na misokoto 300 ya bangi, Aprili,2014.

Kwa mujibu wa watu waliokuwa katika eneo la mahakama hayo, mahabusu hao walikuwa wakipaza sauti kupinga madaraja(ubaguzi) miongoni mwa watuhumiwa, wenye uwezo kifedha na wasio nacho, hali ambayo imesababisha wengine kuachiwa na wengine kuendelea kusota magerezani kwa kisingizio cha "upelelezi haujakamilika"

Mahabusu hao walisikika wakipaza sauti kutoka ndani ya basi: "Wenzetu hata mwezi haujaisha wanafutiwa kesi, jamani sisi tumekosa nini? Tunataka haki itendeke kwa wote" walisema.

Kuachiwa kwa watuhumiwa wanaolalamikiwa na mahabusu wenzao kunasemekana kumetokana na hatua ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Arusha kubadilisha hati ya mashitaka na hivyo kuwawezesha kupata dhamana.

Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa ofisi yake haina taarifa za watuhumiwa hao kupewa dhamana lakini alisema kulikuwa na jaribio la kufanya hivyo.

Bwana Nzowa amesema baada ya kubainika njama hizo, ofisi yake ilipinga, akisema kuwa kosa la watuhumiwa lilikuwa wazi na hivyo kuonyesha hali ya kutoamini kuwa watuhumiwa wanaweza kupata dhamana kwa kosa hilo!

Hata hivyo Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, DPP haijaweza kulitolea maelezo suala la mahabusu hao kulalamikia mahabusu wenzao kupendelewa katika utoaji wa haki kwa makosa wanayotuhumiwa.