Nigeria: Polisi waahidi dola laki 3

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kundi la Boko Haram limekiri kuwateka nyara wasichana hao na kusema kuwa litawauza

Polisi nchini Nigeria wameahidi kumtunuku dola laki tatu za marekani yeyote atakayetoa habari zitakazowasaidia kuwapata zaidi ya wasichana mia mbili waliotekwa na kundi la wapiganaji wa boko haram mwezi uliopita .

Juma lililopita Wapiganaji wa Boko Haram walisema kuwa wasichana hao 200 kutoka eneo la Chibok waliotekwa mwezi uliopita watauzwa.

Aidha Maafisa nchini Nigeria Wamesema kuwa idadi ya wasichana zaidi waliotekwa nyara na kundi la wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram imetimu 11.

8 kati yao walitekwa kutoka kijiji cha Warabe kilichoko katika jimbo la Borno siku ya jumapili nao watatu zaidi wakatekwa kutoka kijiji jirani .

Rais wa Marekani ameingilia swala hilo akisema kuwa serikali yake itatoa msaada ili kuwakomesha wapiganaji hao.

Tayari marekani imewatuma maafisa kadhaa kusaidia kusuluhisha kwa amani kitendawili cha utekaji nyara huo.