Chama cha ANC mbele kwa kura

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Licha ya kashfa nyingi, kiongozi wa chama cha ANC Jacob Zuma bado ana ushawishi mkubwa

Wakuu wa tume ya uchaguzi nchini Afrika-Kusini wametangaza kuwa shughuli ya kuhesabu kura inaenelekea kukamilika baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika juzi kwa mara ya tano tangu utawala wa mwafrika mzungu.

Chama tawala cha ANC kinaongoza kwa zaidi ya asilimia 63, huku kile cha Democratic Alliance kikiwa na asilimia 23.

Chama kipya cha Economic Freedom Fighters cha Julius Malema kikiwa katika nafasi ya tatu.

Jumla ya asilimia 96 ya kura zilizopigwa zimehesabiwa.

Mwandishi wa BBC Andrew Harding anasema kuwa ukosefu wa ajira,ufisadi na ukosefu wa usawa katika jamii ni changamoto kubwa lakini wapiga kura bado wana imani na chama cha ANC.

Tume ya uchaguzi imesema kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani katika maeneo mengi ya nchi huku asilimia 73 ya wapiga kura wakijitokeza kupiga kura.

Uchaguzi huu ni wa kwanza tangu nchi hiyo kuondokewa na rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo hayati Nelson Mandela. Afrika Kusini imetimiza miaka 20 tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu.

Idadi kubwa ya wananchi imekuwa ikilalamikia utenda kazi wa serikali hasa kwa kuwa kuna kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira.

Wadadisi wanasema kuwa chama cha ANC huenda kikatumia fursa hii kuimarisha uchumi wa nchi hasa baada ya miaka mitano ya kile kinachosemekana kuwa utawala mbovu wa Rais Jacob Zuma.