Balozi wa Malawi afariki dunia Tanzania

Image caption Bendera ya Malawi

Balozi wa Malawi nchini Tanzania Bi Flossie Gomile Chidyaonga amefariki dunia mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam akipelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi zaidi kutokana na matatizo ya maradhi yaliyokuwa yakimkabili.

Taarifa ya wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania kwa vyombo vya habari imesema "Balozi Chidyaonga aliyekuwa na umri wa miaka 54 amefariki Ijumaa kutokana na mshipa mkuu wa AORTA kuvimba na kupasuka kulikosababisha damu kukusanyika kwenye mfuko wa moyo na hivyo kufanya moyo ushindwe kufanya kazi."

Wizara hiyo imesema, katika kipindi chote alichokuwa mwakilishi wa Malawi nchini Tanzania, Balozi Chidyaonga alifanya kazi yake ya kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya nchi mbili hizo kwa umahiri wa hali ya juu.

Mwili wa marehemu Balozi Chidyaonga unatarajiwa kusafirishwa Jumanne kwenda Malawi na Jumatano mazishi yamepangwa kufanyika huko Blantyre.