Mchwa wavamia ikulu Paraguay

Image caption Mchwa wavamia ikulu ya Paraguay

Mchwa wamevamia makaazi rasmi ya rais wa Paraguay na kutishia udhabiti wa jengo hilo.

Watalamu wa maswala ya ujenzi wameonya kwamba huenda Rais huyo akapoteza makaazi yake iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kuwaangamiza mchwa.

Kwa mujibu wa wanasayasi wa kibiolojia mchwa ni mdudu mwenye bidii sana na kamwe hachoki kutekeleza majukumu yake.

Na ni kutokana na hilo ndipo wahenga katika juhudi za kutoa motisha kwa yeyote yule anayetaka kufanikiwa maishani wakasema ''lazima awe na bidii ya mchwa''.

Msemo huu umedhihirika nchini Paraguay baada ya habari kwamba mchwa wamevamia makaazi rasmi ya Rais Horacio Cartes.

Wataalam wa maswala ya ujenzi wanasema mchwa hao wameharibu sakafu na sehemu zilizojengwa kwa mbao.

Wahandisi hao wameonya kuwa huenda sehemu moja ya jengo hilo likaanguka iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Wamependekeza Rais huyo ahamishwe kutoka jengo hilo ili wataalam waweze kupambana na wadudu hao wenye bidii na ukarabati uweze kufanyiwa jengo hilo.

Ni dhahiri kuwa wageni hao waharibifu sasa wanatishia starehe na itifaki ya Rais Horacio Cartes.