Ukraine:Umoja wa Mataifa kutoa ripoti

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ukraine:Umoja wa Mataifa kutoa ripoti

Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuzindua ripoti kuhusu ukiukwaji wa haki za haki za binadamu nchini Ukraine.

Ripoti hii itakuwa ya pili kutolewa tangu mwezi Machi.

Ripoti hii inatolewa wakati machafuko yakiendelea kushuhudiwa mashariki na kusini mwa Ukraine ambapo makundi yanayounga mkono serikali ya Urusi yanashtumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Makundi hayo ambayo yanapigania kujitenga kutoka Ukraine,awali yalilaumu majeshi ya serikali ya Ukraine kwa kusababisha vifo vya watu waliokuwa wameteka makao makuu ya majimbo ya mashariki.

Kundi la wachunguzi 34 wa haki za binadamu wamepelekwa katika maeneo mbalimbali ya Ukraine kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadam katika juhudi za kujaribu kutuliza hali ya taharuki.

Ripoti ya kwanza iliyochapishwa mwezi Aprili ilisema machafuko nchini Ukraine yamechochewa na matatizo kadhaa yakiwemo ufisadi ndani ya serikali, ubaguzi dhidi ya makabila yenye watu wachache na chuki inayosababishwa na uchochezi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ukraine:Umoja wa Mataifa kutoa ripoti

Ripoti hii mpya inatarajiwa kuangazia ghasia za hivi karibuni hasa katika maeneo ya Odessa, Donetsk na Mariupol.

Kamishna wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay ametoa wito kwa pande zote kuacha chuki na mapigano na kuonya kuwa huenda hali nchini Ukraine ikafikia kiwango kisichoweza kudhibitiwa.

Urusi imekuwa ikilaumiwa kwa kuchochea ghasia mashariki na Kusini mwa ukraine kwa kuunga mkono makundi yanayotaka kujitenga.

Serikali kwa upande wake imekiri kuwa maafisa wake ndio wakulaumiwa katika vifo vya watu waliochomeka hadi kufa katika majengo ya serikali yaliyowashwa moto majuma kadha yaliyopita.