Bado tuko ngangari uongozini - Libya

Haki miliki ya picha n
Image caption bunge la Libya

Serikali ya Libya imesisitiza kuwa bado imedhibiti uongozi wa nchi.

Hii ni hotuba ya kwanza kutoka kwa serikali hiyo tangu kutokea mapigano katika mji mkuu Tripoli siku ya Jumapili.

Maafisa wanasema kuwa watu 2 wameuawa na wengine zaidi ya 55 kujeruhiwa katika mapigano hayo ambayo ni ya punde zaidi. Mapigano hayo yalizuka kufuatia taarifa kutoka kwa kikundi kilichojiteuwa kuwa jeshi la kitaifa, ambacho kilivamia na kuvuruga kikao cha bunge.

Katika hotuba kwa taifa kupitia televisheni, waziri wa haki wa Libya salah Al-marghani alishutumu shambulio hilo dhidi ya bunge la nchi hapo Jumapili. Alitoa wito wa kusitishwa uhasama huo na kufanyika mashauriano ya kitaifa huku akisisitiza kuwa bado serikali inaendelea na majukumu yake.

Tisho kwa utawala

Taarifa ya awali kutoka kwa mpiganaji wa kundi la Zintan ilionya kuwa kundi hilo litafanya juhudi zote kulivunja bunge la nchi na kukabidhi majukumu ya kuongoza shughuli za serikali kwa baraza la katiba.

Hata hivyo bado haijabainika iwapo baraza hilo limefahamishwa juu ya mipango hiyo. Pia amesema kuwa matukio ya Jumapili iliyopita hayalengi kufanya mapinduzi katika nchi.

Wapiganaji wa Zintan walishambulia kwa muda mfupi jengo la bunge na muda mfupi baadaye kurejea katika kambi zao. Baadaye walikabiliana vikali na kundi hasimu la wapiganaji ambalo halikutambuliwa.

Mwanasiasa wa chama cha Liberal National Forces Alliance party, Tawfik Breik, ameelezea wasiwasi kuwa nchi yake sasa imegeuzwa kuwa volcano inayosubiriwa kulipuka.

''Hapa nchini Libya hakuna tena bunge. Hakuna serikali ya kweli. Kila mahali kuna makundi ya wapiganaji.'' Amesema bwana Tawfik. Pia ameongeza kuwa hawana matumaini ya maisha kwani ni wazi kifo kinawasubiri. '' Tunajua italipuka hivi karibuni na sote tutakufa kwasababu hakuna muongozo katika nchi hiii. Hakuna kabisa!''