Waasi wa Seleka CAR waapa kujizatiti

Wapiganaji CAR Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji waasi CAR

Kundi la waasi wa Seleka katika Jamuhuri ya Afrika ya kati linasema limejizatiti upya kwa ajili ya udhibiti thabiti wa wapiganaji wake.

Serikali imelaani hatua hiyo, ikisema kundi hilo limechukua mali za jimbo katika eneo la kaskazini mwa nchi.

Waasi hao ambao wengi wao ni waislam wamekuwa wakihusika katika mapigano makali na kundi la wapiganaji wakristo maarufu kama anti-balaka tangu mwezi Machi mwaka 2013.

Mzozo huo umesababisha kusambaratika kwa takriban asilimia 25% ya wakazi wa Jamuhuri ya Afrika ya kati milioni 4.6.

Umoja wa Afrika, Ufaransa na Muungano wa Ulaya wamepeleka kikosi cha askari elfu 7,000 wanaopigania kuhakikisha mzozo huo unamalizika.

Mratibu wa Seleka Abdoulaye Hisseine amesema kundi hilo limeweka muundo mpya wa utawala wa wapiganaji hao kuwaongioza wapiganaji hao kaskazini mwa taifa hilo.

" Unataka sisi tupoteze wapiganaji hawa wote wa Seleka , bila kuwa na mpango wowote wa kuwaangalia? kama ni hivyo ni sawa sasa. Kama si hivyo, hiyo ndio njia pekee ya kuwaweka chini ya udhibiti " alisema .

Mchambuzi wa BBC wa idhaa ya kifaransa Abdourahmane Dia amesema wapiganaji wa Seleka bado wanadhibiti eneo kubwa la Kaskazini mwa CAR, na baadhi ya maeneo ya kati mwa taifa hilo, licha ya kupoteza mamlaka mwezi Januari.