Uchumi wa Ethiopia unaimarika kwa kasi

Haki miliki ya picha
Image caption Dola bilioni nne za kimarekani kwa miundo msingi Ethiopia

Miaka thelathini baada ya Ethiopia kukabiliwa na njaa iliyowauwa raia wengi, nchi hio ambayo ilitambulika kwa umaskini wa kukithiri sasa imeimarika na kuwa moja wapo ya nchi yenye uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi barani Afrika.

Ethiopia sasa imeanzisha mradi wa maendeleo wa kuboresha miundo mbinu ili kuinua maisha ya watu millioni 90 wa nchi hiyo.

Uchumi wa Ethiopia umeimarika katika kipindi cha miaka saba iliyopita huku shirika la fedha duniani, IMF likisema viwango vya ukuaji vimeongezeka kwa asilimia saba kila mwaka.

Na ni katika sekta ya ujenzi ambapo ukuaji huo umeshuhudiwa zaidi.

Haki miliki ya picha
Image caption Ethiopia inajitahidi kuimarisha miundo mbinu

Maendeleo nchini

Ujenzi wa majumba makubwa, maeneo ya burudani na nyumba za wapangaji umeongezeka pakubwa.

Aidha ujenzi wa miundo msingi pia umetiliwa maanani. Mwaka huu pekee, serikali ya Ethiopia imetenga takriban dola bilioni nne za kimarekani kwa ajili ya ujenzi huo.

Waziri wa fedha nchini humo, Sufian Ahmed anasema serikali itaendelea kuwekeza katika barabara na reli.

Tayari ujenzi wa reli katika mji mkuu wa Addis Ababa, umeanza na unatarajiwa kukamilishwa mwaka ujao.

Mradi huo utagharimu takribani dola milioni mia tano.

Haki miliki ya picha
Image caption Changamoto hazikosekani katika kukuwa kwa uchumi huo

Changamoto

Licha ya hatua hizo, viwango vya umaskini ni vikubwa Ethiopia na serikali imeendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika kupambana na mfumuko wa bei za bidha muhimu.

Ni suala ambalo waziri Ahmed anasema serikali inalitilia maanani.

Licha ya Ethiopia kukabiliwa na changamoto hizo, inasema imo katika mkondo wa kuwa taifa lenye utajiri wa kadri kufikia mwaka wa 2025.