Van Gaal apania kushinda taji la premia

Image caption Louis van Gaal anapania kushinda taji la ligi kuu ya premia

Kocha mpya wa Manchester United , Louis van Gaal anapania kushinda taji la ligi kuu ya premia ya Uingereza katika mwaka wake wa kwanza tangu achukue usukani Old Trafford.

Van Gaal anajibunia rekodi ya kutwaa taji la ligi katika mwaka wake wa kwanza alipoiongoza Barcelona kutwaa taji la Uhispania msimu wa 1997-98 na kisha akarejelea tena ushindi akiiongoza Bayern Munich ya Ujerumani mwaka wa 2009-10. Iwapo atafaulu van Gaal atajiunga na makocha wengine watatu Jose Mourinho na Carlo Ancelotti wa Chelsea na Manuel Pellegrini wa Manchester City.

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya kitaifa huko Uholanzi RTL van Gaal mwenye umri wa miaka 62 alisema itakuwa bora iwapo Manchester Utd itarejea kileleni Uingereza.

Van Gaal, ambaye ameandikisha kandarasi ya miaka mitatu amewahi kushinda mataji saba tofauti akiwa na vilabu vinne tofauti - Ajax, Barcelona, AZ Alkmaar na Bayern Munich.

United ilimaliza katika nafasi ya 7 katika msimu uliokamilika wa 2013-14 na ikashindwa kufuzu kwa michuano ya bara ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25.