Watu 35 zaidi waagizwa kuripoti Thailand

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Raia wakiandamana nchini Thailand ili kupinga mapinduzi ya kijeshi nchini humo.

Serikali mpya ya jeshi nchini Thailand imewaagiza watu 35 zaidi wakiwemo watu maarufu na wasomi kuripoti mbele yake katika kipindi cha masaa kadhaa.

Siku ya ijumaa ,serikali hiyo ya kijeshi iliwaagiza wanasiasa 155 kutoka pande zote mbili za kisiasa kufika mbele yake mara moja.

Miongoni mwa wale waliofika mbele yake na kuzuiliwa ni aliyekuwa waziri mkuu Yingluck Shinwatra.

Msemaji wa jeshi amesema kuwa kuzuiliwa kwake hakutadumu zaidi ya juma moja,lakini ni muhimu huku mambo nchini humo yakirekebishwa.

Wale waliodinda kufika mbele ya serikali hiyo mpya siku ya ijumaa wamepewa masaa machache kujiwasilisha.

Marekani imesema kuwa inaahirisha msaada wa kijeshi wa dola nusu millioni kwa Thailand,lakini haijasitisha ushirikiano wa mazoezi ya kijeshi kati yake na taifa hilo.