Malaysia yatoa data kuhusu MH370

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Picha ye ndege ya Malaysia iliyopotea pamoja na ujumbe kwa wale waliofariki katika ajali ya MH370

Serikali ya Malaysia, imetoa data iliyotumika kuthibitisha kuwa ndege ya Malaysia iliyotoweka MH370 ilianguka kusini mwa bara Hindi.

Data hiyo ilitolewa kwanza kwa jamaa wa abiria wa ndege hiyo ambao wamekuwa wakitaka maafisa wakuu kutoficha taarifa zozote kabla ya vyombo vya habari kutoa taarifa hiyo.

Data hiyo iliyotolewa Jumanne,ni ya kurasa 47 pamoja na maelezo mengine kutoka kwa kampuni ya uingereza ya Inmarsat.

Ndege ya MH370 ilitoweka tarehe 8 mwezi Machi, ilipokuwa safarini kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing.

Ilikuwa imewabeba watu 239 wengi wakiwa raia wa Uchina.

Tangu kupotea , ndege hiyo haijaonekana na hakuna sababu iliyotolewa ya kupotea kwa ndege yenyewe.

Data iliyotolewa inaonyesha mawasiliano ya kawaida kati ya marubani na na mtambo wa Satelite ambayo yaliwasababisha wachunguzi kufikia kuwa ndege hiyo ilimaliza safari yake nchini Australia.

Wakati huohuo, msako wa chini ya bahari kuitafuta ndege hiyo kwa kutumia Manowari ya Roboti, bado unaendelea mjini Perth, Australia.

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Wafanyakazi wa kituo cha mawasiliano ya Satelite nchini Uingereza

Manowari hiyo imekabidhiwa kwa Australia kwa mkopo.

Kadhalika manowari yenyewe kwa jina Bluefin-21, ambayo ina uwezo wa kuona vifaa vidogo sana chini ya bahari, ilianza tena kazi yake wiki hii baada ya kupatwa na hitilafu na kurekebishwa.

Inatarajiwa kuondoka katika eneo hilo Jumatano na kurejea kwa kazi tena tarehe 31 mwezi Mei.

Manowari hiyo ilimaliza shughuli za mwanzo kutafuta ndege hiyo baada ya taarifa za kuwepo vinasa sauti vya ndege hiyo iliyotoweka baharini ingawa havikupatikana.

Serikali ya Australia sasa inajiandaa kwa msako mwingine chini ya bahari kwa kutumia vifaa maalum vilivyokodiwa.