Wahamiaji wahamishwa Ufaransa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wahamiaji hao, wamekuwa wakijaribu kuvuka mpaka kuingia nchini Uingereza

Polisi mjini Calais, Kaskazini mwa ufaransa, wamewatimua wahamiaji 800 kutoka Asia , Mashariki ya Kati na Afrika wanaoishi katika eneo lililo karibu na bandarini ambako wamekuwa wakipiga kambi

Maafisa wanasema kuwa hatua ya wanajeshi kuwatimua wahamiaji ni muhimu ili kuweza kukabiliana na mlipuko wa ugongwa wa Upele ambapo idadi ya walioambukizwa imeendelea kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Polisi walizingira makazi duni ya wahamiaji hao na kuanza kuwaondoa kwa nguvu baada ya muda waliopewa kuondoka katika eneo hilo kuisha.

Wahamiaji hao, wamekuwa wakijaribu kuvuka mpaka kuingia nchini Uingereza na wanasema kuwa hawana mahali pengine pa kuenda baada ya kambi zao kuharibiwa.

Polisi waliofika kuwaondoa wahamiaji hao, wamekuwa katika makabiliano ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanaopinga kuondolewa kwa wahamiaji hao kutoka eneo hilo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wengi wa wahamiaji huataka kuingia Uingereza wakisema hali huko ni afadhali

Wengi wa wahamiaji hao hata hivyo wameamua kuhama na kutafuta mahali opengine pa kuishi.

Mwanamume mmoja raia wa Eritrea alisema kuwa amejaribu kuingia nchini Uingereza kwa kutumia malori yanayovukisha mizigo ingawa hajafaulu hata hivyo hajafa moyo kwani amesema ataendelea kujaribu.

Watu wengi katika kambi hizo wanaamini kuwa Uingereza ni mahala afadhali kwao kuishi ikiwa wataweza tu kuvuka na kuingia nchini humo.

Mnamo mwaka 2002, serikali ya Ufaransa ilifunga kituo cha Red Cross kilichokuwa kinawahudumia wahamiaji hao , lakini wakimbizi hao wakaanza kujenga kambi za muda ambazo wanaishi ndani.