Viongozi wa EU kujadiliana ajenda mpya

Haki miliki ya picha
Image caption Rais wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Ulaya Herman Van Rompuy, akihutubia mkutano Brussels.

Viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wamekubaliana kuchunguza upya ajenda ya muungano huo baada ya wapiga kura "kutoa ujumbe mzito", Rais wa Baraza Kuu la Ulaya, Herman Van Rompuy amesema.

Bwana Van Rompuy alisema kuwa viongozi wa mataifa 28 wanachama walikuwa wamemwuliza kaunzisha mashauriano juu ya uongozi wa siku za usoni za muungano huo.

Alisema hayo baada ya mkutano uliofanyika mjini Brussels kujadiliana matokeo ya uchaguzi ambapo makundi ya mrengo wa kulia yalionekana kupiga hatua kubwa ambapo walipata viti vingi zaidi Bungeni, kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Matokeo ya uchaguzi wa Bunge la jumuiya ya Ulaya umelazimisha wanachama kuchunguza upya kwa nini viongozi wa sasa walishindwa pakubwa katika maeneo yao.

Licha ya ushindi wa makundi kadhaa yanayopinga muungano wa Ulaya, kwa ujumla watu wanaopenda muungano wa Ulaya walishinda katika uchaguzi huo.

Mkutano wa viongozi wanachama mnamo Jumanne ulikuwa nafasi ya kwanza kwa viongozi wote kujadiliana hatua ya kuchukua baada ya uchaguzi wa juma lililopita.

Mwandishi wa BBC amesema kuwa baadhi ya mabadiliko yanayotarajiwa ni pamoja na kupunguza usimamizi na mikakati ya kuimarisha uchumi katika mataifa mbalimbali