Uchumi wa Afrika kupigwa msasa Msumbiji

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mkurugenzi mkuu wa IMF, Christine Lagarde.

Shirika la fedha duniani IMF leo linazindua kongamano la ngazi ya juu kuzungumzia maswala ya ukuaji wa Uchumi barani Afrika.

Kikao hicho kwa jina "Africa is rising" kitafanyika katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo.

Japo vita na majanga asili barani Afrika vimegonga vyombo vya habari katika muda wa miaka mitano iliyopita, kimya kimya baadhi ya nchi nchi za Kiafrika zimeshuhudia ukuaji mkubwa wa kiuchumi.

Shirika la IMF linakadiria kuwa ukuaji wa kiuchumi wa kati ya asilimia 5 na 6 utaendelea kushuhudiwa katika miaka michache ijayo. Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Christine Lagarde, amesema viwango hivyo ni vya kuridhisha lakini ameonya kwamba viwango vya umaskini bado viko juu sana.

Amesema mojawapo ya matatizo makubwa yanayokumba nchi za Afrika ni pengo lililopo kati ya matajiri na maskini. Kwa mujibu wa IMF ukuaji wa kiuchumi unaodhihirika kwa kiwango kikubwa umechangiwa na ongezeko la biashara ya malighafi kutoka Afrika kama vile mafuta na vyuma.

Japo biashara ya malighafi huchangia pakubwa katika uchumi wa mataifa, mapato hayo hayafikii wananchi wa kawaida.

Kutokana na hilo mkutano wa IMF mjini Maputo uliopewa jina ''Africa Rising'' utalenga zaidi mbinu za kufikia ukiaji wa kiuchumi unaoshirikisha jamii kikamilifu na jinsi bora ya kusimamia mali asili.