China yataka watoto wengi zaidi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Serikali-Kila Mchina sasa ruhsa kuzaa zaidi ya mtoto mmoja

Uchina imeanza kulegeza sheria zake za mpango wa uzazi, na sasa inapiga kampeni yenye lengo la kuongeza angalau watoto millioni mbili zaidi wanaozaliwa kila mwaka.

Serikali itaongeza wakunga na wahudumu sambamba na kupanua nafasi hospitalini na kuongezwa idadi ya vitanda na vifaa nyenginevyo.

Kwa mda mrefu Uchina imeendeleza sera kali ya mpango wa uzazi ya kulazimu familia kuwa na mtoto mmoja tu huku wanaokiuka wakichukuliwa hatua kali jambo linaloshutumiwa kimataifa.

Lakini mwaka jana serikali iliianza kulegeza kamba kwa kusema iwapo mmoja wa wazazi amekuwa mtoto wa pekee katika familia basi anaweza kuzaa mtoto wa pili.

Japo hatua za awali zilichukuliwa kukabiliana na idadi kubwa ya watu nchi humo, sasa kumetokea mapungufu ambayo yanahitaji kusawazishwa.

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption baadhi ya wachina katika kituo cha reli wakisubiri usafiri. Uchina ina idadi kubwa zaidi ya watu duniani zaidi ya watu billioni moja.

Wapanga sera wamependekeza juhudi hizo za kuongeza idadi ya watoto zichukuliwe sasa la sivyo Uchina itajikuta na upungufu mkubwa wa nguvu kazi za vijana,huku idadi ya wazee na wanaostaafu ikiwa kubwa kiasi chakuzorotesha uchumi wa taifa hilo kubwa duniani.Japo bado umaskini unakumba baadhi ya raia wake,Uchina imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi mnamo siku za hizi karibuni na sasa ndilo taifa la pili kwa utajiri duniani,baada ya Marekani.

Hatua hiyo mpya pia huenda ikaleta afueni kwa wengi kwani sera hiyo ya mtoto mmoja kwa familia ilikabiliwa na changamoto nyingi.

Visa na mateso kwa baadhi ya wazazi na watoto huripotiwa huku watoto vilema, wagonjwa au wa jinsia isiyopendelewa na wazazi wao kubaguliwa na kutelekezwa.