Mume amlilia mkewe Pakistan

Image caption Farzana Mohammed Iqbal amelaumu polisi kwa mauaji ya mkewe

Mume wa mwanamke aliyepigwa mawe na familia yake nchini Pakistan amelaumu polisi kwa kupuuza mauaji ya mwanamke huyo, Farzana Parveen.

Mohammed Iqbal - aliambia BBC kuwa alishtushwa na kukasirisha na maafisa wa polisi waliokuwepo karibu na mahali palipotokea kitendo hicho lakini wakakosa kufanya lo lote kunusuru maisha ya mkewe.

"Kilichotokea ni kibaya sana. Mmoja wa jamaa yangu alivua shati na kuwapungia maafisa wa polisi ili waweze kuingilia lakini wakapuuza.Walishuhudia kimyakimya tu Farzana akiuawa na wao hawakufanya lo lote," alisema Iqbal

Waziri mkuu wa Pakistani Nawaz Sharrif ametaka hatua za kisheria zichukuliwe mara moja na ripoti kuhusu ukatili huo itolewe leoleo Alhamisi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamepanga maandamano kulaani kitendo hicho.

Wakati huohuo kamishna wa Umoja wa Mataifa anayesimamia Haki za Kibinadamu, Navi Pillay, amejiunga na maelfu ya watu duniani wanaoshutumu vikali mauaji ya Farzana, aliyeuliwa na wanafamilia yake nje tu ya mahakama alikokuwa wameenda kujaribu kusuluhisha mzozo huo wa kifamilia. Kiini cha mzozo ni madai ya familia ya Farzana kuwa aliolewa na mwanamume aliyempenda lakini wanafamilia hao hawakutaka aolewe na mwanamume huyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, aliyeshutumu mauaji ya mwanamke wa Pakistan.

Mamia ya wanawake huuliwa kila mwaka nchini Pakistan kwa kuolewa na watu wasiopendwa na familia zao, jambo ambalo halikubaliwi katika jamii nyingi ambazo hazipendelei maisha mamboleo yanayotambua watu kupendana kabla ya kuoana.

Makundi mbalimbali ya kupigania haki za kibinadamu kote duniani hutoa wito kwa Serikali ya Pakistan kuhakikisha kuwa wanaoshiriki mauaji kama haya wanashtakiwa; lakini juhudi zao zimeambulia patupu.