Vijana wavamia msikiti CAR

Haki miliki ya picha
Image caption Vijana waliwasha moto magurudumu na kuyaweka barabarani

Kikundi cha vijana wakristo katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, wameharibu msikiti na kuweka vizuizi barabarani kwa kutumia magurudumu ya moto mjini Bangui.

Shambulizi hili limekuja siku moja baada ya wapiganaji wa Seleka, kushambulia kanisa kwa kutumia maguruneti na risasi , huku watu kadhaa wakiuawa.

Waasi wa Seleka ambao ni waisilamu , wamekuwa wakipigana vikali na wapiganaji wakristo wanaojiita 'anti-balaka' tangu mwezi Machi mwaka 2013.

Takriban robo ya watu wote nchini CAR, wameachwa bila makao kutokana na vita.

Hapajakuwa na ripoti zozote kuhusu majeruhi kufuatia mashambulizi dhidi ya msikiti katika mtaa wa Lakouanga mjini Bangui.

Taarifa kadhaa zilisema kuwa msikiti huo ulikuwa bila watu wakati wa mashambulizi.

Msemaji wa jamii ya waisilamu wa Bangui, Ousmane Abakar, aliambia shirika la habari la AP kwamba kwa miezi sita iliyopita,waisilamu wamekuwa wakishambuliwa huku misikiti ikiharibiwa.

Shambulizi la Jumatano dhidi ya kanisa lilisababisha vifo vya watu 15 na lilijiri baada ya mapigano katika eneo la PK5 mjini Bangui.

Kasisi mmoja wa kanisa hilo, Jonas Bekas, alifahamisha BBC kuwa wanajeshi wa kulinda amani waliwasili kuchelewa na kukosa kuzuia mauaji.