Tumbaku 'dhahabu' ya Malawi

Image caption Malawi na Zambia ndio nchi zinazozalisha kiwango kikubwa cha Tumbaku Afrika

Malawi ni miongoni mwa nchi zinazozalisha tumbaku kwa wingi duniani. Uchumi wa nchi hiyo iliyoko kusini mwa bara la Afrika unategemea kilimo cha zao hilo kwa asilimia 75.

Ikiwa leo ni siku ya kutovuta tumbaku duniani, Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza yupo nchini humo na anasema kila unapopita mitaani kwenye miji mikubwa ya Lilongwe na Blantyre na hata maeneo ya vijijini hakuna tofauti.

Wavutaji wa tumbaku na hasa sigara hawana haja ya kujificha ama kujistiri ili kuwalinda wasiovuta wasidhurike na moshi wa tumbaku.

Malawi ni kati ya nchi zenye sheria ya kuzuia watu wasivute sigara hadharani na hata matangazo ya biashara ya sigara hayaruhusiwi, lakini kama ilivyo kwa baadhi ya nchi zingine, sheria hizo hazisimamiwi kabisa.

'Mhimili wa uchumi wa nchi'

Tumbaku ndiyo dhahabu ya Malawi, wenyewe wanasema bila tumbaku hakuna maisha

Kijana mmoja amezungumza na BBC akasema yeye havuti sigara na anafahamu vizuri madhara ya kuvuta sigara, lakini wao kama nchi hawawezi kuacha kulima tumbaku kwani ndiyo msingi wa uchumi wa Malawi, na hawana bidhaa nyingine mbadala ya kufidia kilimo cha tumbaku itakapobidi kuacha kulima zao hilo.

Wamalawi walioko mashambani na hata mijini kwa umoja wao bila kujali wasomi ama mbumbumbu, wana kitetea kilimo cha tumbaku kwa nguvu zote.

Mkulima wa zao hilo Amon Ndewere ambaye anamiliki shamba la ekari 40 anasema kelele za ulimwengu kupiga vita kilimo cha tumbaku kwao hazina tija kabisa wanachoangalia ni jinsi gani wanunuzi na serikali watawaboreshea maisha yao bila kuwanyonya.

'Tumbaku inauzwa kwa mnada

Image caption Wauzaji wa Tumbaku mnadani

Wakulima wa tumbaku nchini Malawi hawaruhusiwi kuuza wenyewe tumbaku yao kwa namna yoyote, bali wanapaswa kujiunga pamoja kwenye vikundi vidogo vidogo na kuipeleka kwenye mnada maalum wa tumbaku unaosimamiwa na shirika la Umma Auction Holdings.

Huko wanakutana na wanunuzi ambao ni makampuni makubwa ya kimataifa kama Alliance One, Japan Tobacco, Malawi Leaf na mengine.

Afisa mtendaji Mkuu wa Tume ya udhibiti wa tumbaku nchini Malawi Bruce Muthali, Anasema kazi yao ni kusimamia sera ya zao hilo listawi kwa manufaa ya nchi na watu wake.

'Tumbaku ya kipekee duniani'

Image caption Tumbaku ndio dhahabu ya Malawi kama wanavyosema wenyewe

Malawi ni mzalishaji pekee duniani wa tumbaku inayoitwa kwa jina la kitaalam Burley, ambayo huchanganywa na tumbaku zingine ili kupata mchanganyiko bora wa sigara.

Na kwa hakika nchi hii haijaathirika kwa lolote kwenye kilimo cha zao hili isipokuwa tu misukosuko ya kawaida ya kupanda na kushuka kwa bei ya tumbaku kwenye soko la dunia.

Inaelezwa kuwa Malawi kuna wavutaji wengi wa sigara, lakini serikali ilifunga kiwanda chake cha kutengeneza sigara zaidi ya miaka 15 iliyopita,na sasa kuna kiwanda kidogo tu kimoja, sigara zote zinazopatikana nchini humo zinatoka nchi jirani na hasa Zambia na Msumbiji huku Tanzania na Afrika Kusini zikichangia ongezeko kidogo sana.

Image caption Nchini Malawi matangazo ya kibiashara ya Sigara hayaruhusiwi

Waswahili wanasema kimfaacho mtu chake! Malawi inategemea zaidi tumbaku kuliko bidhaa nyingine yoyote, swali kwa walimwengu ni jinsi gani itaachana na kilimo hiki.. kwa sababu tu wataalamu wanasema tumbaku ina madhara.