White House yashutumu silaha za Urusi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Barack Obama akizungumzia hali ya vita nchini Ukraine akiwa Ikulu ya White House.

Ikulu ya White House imeeleza masikitiko yake kuhusiana na wapiganaji waasi wanaoungwa mkono na Urusi Mashariki mwa Ukraine kuwa wanatumia silaha kubwa katika makabiliano nchini humo.

Taarifa hiyo imetolewa mapema Alhamisi baada ya helikopita ya kijeshi ya Ukraine kudunguliwa na bunduki kubwa ya kuangusha ndege za kurusha makombora ambapo wanajeshi 12 walifariki.

Na Rais Mteule wa Ukraine Petro Poroshenko ameapa kuwaadhibu "majangili" baada ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi kuangusha helikopta ya kijeshi na kuwaua watu 12.

"vitendo hivi vya uhalifu vya maadui wa watu wa Ukraine havitapita bila kuadhibiwa mtu," alinukuliwa kusema na shirika la habari la Unian.

Helikopta ilidunguliwa karibu na jiji la Mashariki la Sloviansk. Jemedari mmoja alikuwa miongoni mwa waliouliwa.

Kumekuwa na mapigano makali kati ya waasi na wanajeshi wa Ukraine katika Slovianski.

"Leo vijana wetu waliuawa kikatili," Bwana Poroshenko alisema Alhamisi.

"Huu ni wakati wa masikitiko makubwa na nawatumia risala zangu za dhati familia na jamaa za wote waliopoteza maisha yao."

Urusi imekariri wito wake kuwa Ukraine inapaswa kusitisha kampeni zake za kijeshi dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi ili "kuanzisha mashauriano kamili ya kitaifa."

Katika tukio tofauti, Ukraine, Urusi na Ulaya zinatazamiwa kuanzisha awamu mpya ya mashauriano mjini Berlin ambako watajadiliana juu ya mzozo unaohusu usambazaji wa gesi ya kutoka Urusi nchini Ukraine.

Kampuni ya gesi ya Urusi ijulikanayo kama Gazprom imeisha kukatisha gesi inayoelekea Ukraine iwapo haitalipa deni kubwa linalokabili taifa hilo.